Serikali kortini kwa kiwanja alichomilikishwa hayati Sokoine

Dar es Salaam. Mfanyabiashara Al- Hussein  Dhanani ameiburuza mahakamani Serikali na Balozi Joseph Edward Sokoine,  mtoto na mwakilishi wa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, hayati Edward Sokoine, kutokana na mgogoro wa kiwanja alichomilikishwa hayati Sokoine.

Kutokana na mgogoro wa umiliki wa kiwanja hicho namba 119 kilichoko Jangwani Beach, wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, mfanyabiashara huyo amefungua shauri la maombi ya zuio kabla ya kesi ya msingi,  Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi.

Amefungua shauri hilo dhidi ya Kamishna wa Ardhi, Msajili wa Hati, Katibu Mkuu wa Wizara Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,  Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Wakili Mkuu wa Serikali (SG)  na Balozi Sokoine, kufuatia notisi ya siku 90 aliyoitoa ya kuishtaki Serikali.

Katika shauri hilo namba 25944/2024, anaiomba mahakama hiyo itoe amri ya zuio la muda dhidi ya wadaiwa, wawakilishi au wakala wao kutokufanya jambo lolote katika kiwanja hicho, mpaka atakapofungua kesi yake, baada ya kumalizika kwa siku hizo 90 za notisi kisheria.

Katika hati ya dharura, iliyoambatanishwa na hati ya maombi, Wakili wake Jerome Msemwa amesema kuwa shauri hilo lina udharura mkubwa na linahitaji kusikilizwa kwa haraka, kwa kuwa mali za mteja wao ukiwemo ukuta aliokuwa ameujenga kuzunguka kiwanja hicho, zimeanza kuvunjwa.

Dhanani katika kiapo chake kinachounga mkono maombi hayo, anadai kuwa yuko katika hatari ya kupata hasara isiyoweza kufidiwa kwani Balozi Sokoine ameanza kubomoa nyumba na wigo wa ukuta kuharibu ushahidi.

Pia anadai kuwa Balozi Sokoine ameanza mchakato wa mazungumzo na wanunuzi wa kiwanja hicho, jambo ambalo litamzuia au kumpa usumbufu katika kutafuta haki yake dhidi ya upande wa tatu, kama amri ya zuio kabla ya kesi ya msingi haitatolewa.

Shauri hilo linalosikilizwa na Jaji Arafa Msafiri lilipangwa kusikilizwa Alhamisi Novemba 14, 2024 lakini halikusikilizwa kwa kuwa jaji Msafiri hakuwepo kutokana na sababu za kiafya. Hivyo liliahirishwa na Jaji Lusungu Hemed hadi  Desemba 10, 2024 saa 3:00 asubuhi litakaposikilizwa.

Katika notisi yake mfanyabiashara huyo anaeleza kuwa atachukua hatua hiyo kwa  madai ya maofisa hao wa Serikali kufanya udanganyifu katika kubatilisha umiliki wake katika kiwanja hicho na kummilikisha hayati Sokoine, kupitia mwakilishi wake, Balozi Sokoine.

Katika notisi hiyo ya Oktoba Mosi 2024, iliyosainiwa na mawakili wake, Jerome Msemwa, Anna Marealle na Godfrey Silayo, ameeleza kusudio la kuchukua hatua hiyo baada ya siku 90 za kisheria kumalizika kama hatakuwa amerejeshewa umiliki wa kiwanja hicho.

Kwa mujibu wa notisi hiyo na kiapo chake Dhanani amekuwa mmiliki wa kiwanja hicho tangu Juni 16, 1994, kwa hati namba 30606.

Hata hivyo alishangaa kubaini kuwa umiliki wake ulishabatilishwa na kisha kumilikishwa kwa hayati Sokoine kupitia kwa mwakilishi wake, Balozi Sokoine, kuanzia mwaka 2021, ikiwa ni miaka 37 baada ya kifo chake, katika mazingira tata.

Kulingana na nyaraka alizoziwasilisha mahakamani awali kiwanja hicho kilikuwa kinamilikiwa na Alassaru Edward Sokoine tangu Novemba Mosi, 1983 kwa hati namba 30606.

Tangu mwaka 1988 Alassaru alikuwa ameshaomba mara kadhaa vibali vya ujenzi, lakini alikuwa akikataliwa kwa sababu za kiusalama kutokana na kiwanja hicho kuwa karibu na eneo la jeshi la mazoezi ya kulenga shabaha.

Hata hivyo Aprili 22, 1994, Alassaru alipewa kibali cha ujenzi, lakini  Juni 16, 1994 alimuuzia mfanyabiashara huyo, Dhanani, akiwa ameshaanza kukiendeleza kwa kujenga makazi ya wahudumu na wigo wa ukuta kwa matofali ya saruji, ambapo pia  aliendelea kukilipia kodi ya ardhi mpaka mwaka 2023.

Mwaka 1999 Dhanani alikiweka dhamana katika Benki ya Exim kwa ajili ya mkopo.

Baadaye alipotaka kuanza mradi wa ujenzi wa jengo kubwa, alipewa notisi ya zuio ya Juni 3, 2006, kama iliyokuwa  imetolewa kwa mmiliki wa awali, Alassaru, mwaka 1988, ikielekeza kusimamisha uendelezaji wowote katika kiwanja hicho mpaka itakapotolewa taarifa zaidi.

Ilieleza  sababu kuwa kiwanja hicho kinapakana na uwanja wa jeshi wa mazoezi ya kulenga shabaha na kuliendeleza yangeweza kusababisha hatari kwa umma, wakati wa mazoezi ya shabaha ya Jeshi.

Hata hivyo wakati Dhanani akisubiri ridhaa kutoka kwa Waziri wa Ulinzi, Julai 19, 2006 alipewa notisi ya siku 90 kutoka kwa Msajili wa Hati katika Wizara ya Ardhi ikieleza kusudio la Wizara kubatilisha haki yake ya umiliki.

Notisi hiyo ilimtaka kutoa maelezo kwa nini kiwanja hicho kilikuwa hakijaendelezwa, na Oktoba 5, 2006 alitoa maelezo kuwa madai ya kutokukiendeleza si sahihi kwa kuwa tayari alikuwa ameshajenga wigo wa ukuta na makazi ya wahudumu.

Pia alieleza kuwa hakuweza kufanya uendelezaji zaidi kutokana na notisi ya zuio iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi, lakini Msajili wa Hati hakuwahi kujibu barua yake wala kumuita kwa ajili ya kujadili suala hilo, licha kuandika barua mbalimbali.

Novemba 4, 2016, Dhanani alipewa barua  na Wizara ya Ulinzi ikimruhusu kuendelea na uendelezaji kiwanja hicho, ambayo pia ilimshauri kuwasiliana na Wizara ya Ardhi kwa vibali vya ziada vinavyotakiwa.

Mwaka 2018 Dhanani akikabiliwa na changamoto kubwa binafsi na za kibiashara ambazo zilimlazimu kusafiri nje ya nchi na alirejea nchini mwaka 2021.

Lakini kabla ya kuendelea na mradi wake wa ujenzi alifanya uchunguzi wa hati ya umiliki kiwanja hicho katika Wizara ya Ardhi na alishangazwa kubaini kuwepo barua iliyoandikwa na Kamishna wa Ardhi kwenda kwake ya Januari 24, 2019 ya kubatilisha umiliki wake.

Barua hiyo ilieleza kuwa hati yake ilikuwa imebatilishwa kwa amri ya Rais ya Januari 18, 2019 kwa madai ya kutokukiendeleza, ambayo hakuwahi kupewa na anayapinga kuwa si sahihi.

Alipofuatilia suala hilo katika Ofisi ya Kamishna wa Ardhi na ya Msajili wa Hati,  alishauriwa na maofisa ardhi kuomba upya umiliki au kurejeshewa kiwanja chake, na akafanya hivyo.

Oktoba 11, 2023 alifanya uchunguzi tena kujua kama hati yake ilikuwa imerejeshwa lakini alibaini kuwa ilikuwa bado inaonekana iko kwa Rais.

Wakati akiendelea kufuatilia kurejeshewa kiwanja hicho, alibaini kuwa kilikuwa kimehamishiwa kwa Joseph Edward Sokoine, kama mwakilishi  wa hayati Edward Moringe Sokoine tangu Mei 17, 2021, wakati ukaguzi alioufanya Oktoba 11, 2023 ulionesha kuwa umiliki wake bado ulikuwa kwa Rais.

Hivyo Dhanani na mawakili wake  wanadai  kuwa mchakato wa ufutwaji na umilikishwaji wa kiwanja hicho kwa Sokoine umegubikwa na kasoro na udanganyifu, uliofanywa kwa nia ovu ya kumpora haki yake.

“Ugawaji wa ardhi ya mteja wetu kwa Joseph Edward Sokoine haukuwa wa haki, ni wa makosa na batili. Kwa heshima tunaomba kwamba hati irejeshee katika jina la mteja wetu,” wameeleza mawakili hao katika notisi hiyo.

Related Posts