BAO moja alilolifunga mshambuliaji wa timu ya taifa, Taifa Stars, Simon Msuva katika ushindi wa timu hiyo wa mabao 2-0 dhidi ya Ethiopia, limemfanya nyota huyo kufikisha mabao 23 na kuifukuzia rekodi iliyowekwa na Mrisho Ngassa mwenye 25.
Msuva aliifungia Stars bao hilo dakika ya 15, huku jingine likifungwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’, katika mchezo wa kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), dhidi ya Ethiopia, uliopigwa juzi kwenye Uwanja wa des Martyrs uliopo jijini Kinshasa DR Congo.
Nyota huyo amefunga mabao 23 katika michezo 93 ya timu ya taifa tangu alipokitumikia kikosi hicho rasmi mwaka 2012, huku akibakisha mawili tu kuifikia rekodi ya Ngassa aliyefunga 25, kwenye mechi 100 alizochezea kuanzia mwaka 2006 hadi 2015.
Mbwana Samatta ndiye anayefuatia kwa ufungaji bora wa timu ya taifa baada ya kufunga mabao 22 katika michezo 82, tangu alipoanza kuichezea mwaka 2011, akifuatiwa na nyota, John Bocco mwenye 16, katika michezo 84, aliyocheza kuanzia 2009.
Hata hivyo, rekodi zinaonyesha nyota anayeongoza kuichezea timu ya taifa michezo mingi ni beki, Erasto Nyoni aliyecheza michezo 107 na kufunga mabao saba tangu alipokichezea kikosi hicho mwaka 2006 hadi 2021 akifuatiwa na Ngassa mwenye 100.
Nyota mwingine anayefuatia ni beki wa kati, Kelvin Yondani aliyecheza michezo 97, ya timu ya taifa bila ya kufunga bao kuanzia mwaka 2008 hadi 2021, akifuatiwa na Simon Msuva mwenye 93, huku John Bocco akiwa ameichezea timu hiyo mara 84.
Beki wa kulia Shomari Kapombe aliyeanza kuichezea timu hiyo kuanzia mwaka 2011, amecheza michezo 83 na kufunga bao moja akifuatiwa na Mbwana Samatta aliyecheza michezo 82, huku kipa, Juma Kaseja akicheza michezo 79, kuanzia mwaka 2002 hadi 2021.
Himid Mao aliyeanza kukichezea kikosi hicho kuanzia mwaka 2013, tayari ameichezea michezo 79 na kufunga mabao mawili tu huku kipa, Aishi Manula akifuatia kucheza michezo mingi baada ya kucheza 65, tangu alipoitwa mara ya kwanza mwaka 2015.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Msuva alisema ni jambo la furaha kwake kuona anazidi kufunga ingawa kitu cha msingi ni kuona timu hiyo inapiga hatua, ili kuyafikia malengo waliyojiwekea ya kuhakikisha kikosi hicho kinafuzu AFCON mwakani.
“Kwanza nichukue nafasi hii kutoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki zetu ambao wamepatwa na majanga ya kudondokewa na jengo Kariakoo, mchezo huu umeisha na sasa tunaweka nguvu mechi ijayo na Guinea ili tutimize malengo yetu kwa pamoja.”