TLS: Tunarudi kwenye misingi na wajibu wetu kwa umma

Arusha. Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimeazimia kurejea kwenye misingi yake ya kuimarisha mchango wake kwa Taifa na wananchi katika masuala ya kisheria.

Azimio hilo limetolewa leo Jumapili, Novemba 17, 2024, na Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi, katika kongamano la maadhimisho ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwa chama hicho.

Akizungumza kwenye kongamano hilo, Mwabukusi ameeleza kuwa maadhimisho hayo yamejikita katika kujadili na kutathmini mchango wa TLS kwa jamii na Taifa, pamoja na kuainisha changamoto zilizopo ili kuimarisha utendaji wao.
Mwabukusi alibainisha kuwa, kupitia majadiliano hayo, TLS inatathmini mchango wake kwa jamii huku ikikiri upungufu uliopo. “Kimsingi tunajaribu kurudi kwenye uwepo wa TLS ili kulisaidia Taifa na kuwasimamia wananchi kisheria, sambamba na kuishauri Serikali kupitia kifungu cha 4 (i) kinachoeleza wajibu wetu kwa umma. Tunataka kuhakikisha kuwa hatua tunazochukua zitaleta maendeleo na ustawi bora kwa Taifa letu,” amesema Mwabukusi.

Amesema TLS ina mchango mkubwa katika masuala mbalimbali, kuanzia kushiriki kwenye kesi muhimu za kihistoria, kama zile zilizomuhusu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, hadi mchango wao katika mabadiliko ya mfumo wa chama kimoja kuwa wa vyama vingi.

Mikakati kusonga mbele
Mwabukusi amegusia changamoto zilizowahi kuikumba TLS, ikiwa ni pamoja na kutishiwa kufutwa kutokana na misimamo yake.

Amesema chama hicho pia kimehusika katika mapendekezo ya mabadiliko ya katiba, ingawa baadhi bado hayajatekelezwa.

Mwabukusi amesema kwa sasa TLS imejipanga kushirikiana na wadau ili kuwafikia na kuendesha mijadala inayolenga kutatua changamoto za msingi za  wananchi, kupitia mpango wa huduma za kisheria.

“Mfano halisi ni changamoto ya watu kupotea katika mazingira yasiyoeleweka. Tunataka vyombo vya ulinzi vitoe taarifa kwa uwazi ili kudhibiti mianya ya watu waovu. Hili linaathiri usalama wa raia na uwekezaji nchini,” amesema Mwabukusi.

Akizungumzia suala la katiba mpya, Mwabukusi amebainisha kuwa TLS inalenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu katiba iliyopo, upungufu wake na maeneo yanayohitaji kuboreshwa.

“Tunaweza kuanza na marekebisho ya msingi badala ya kungoja mchakato mrefu wa katiba mpya. Tunataka kuhakikisha haki za kiraia na kiutawala zinalindwa, mfumo wa uchaguzi unaboreshwa na mahakama zinafanya kazi kwa uhuru na uadilifu,” amesema.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa Bunge la Tanzania kurejea kwenye majukumu yake ya msingi badala ya kutumikia masilahi ya mtu au kundi fulani.

akizungumzia umuhimu wa katiba kutambua na kulinda rasilimali za asili kama misitu, bahari, mbuga za wanyama na madini, Mwabukusi amesema TLS ina wajibu wa kuchangia mawazo ya kitaalamu kuhusu namna bora ya kusimamia rasilimali hizo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Naye mjumbe wa TLS, Ananilea Nkya amesisitiza kuwa uamuzi utakaofikiwa kwenye kongamano hilo, ukitekelezwa ipasavyo utaleta maendeleo makubwa kwa Taifa.

“Haya maamuzi yakitekelezeka, hakika Taifa litakuwa mahali salama kwa uwekezaji na ustawi wa kiuchumi kwa kizazi hiki na vijavyo,” amesema Nkya.

Related Posts