Ushindi waamsha morali ‘Chama la Wana’

KOCHA Mkuu wa Stand United, ‘Chama la Wana’, Meja Mstaafu, Abdul Mingange amesema ushindi wa mabao 2-1, ilioupata timu hiyo dhidi ya African Sports kwenye Uwanja wa kituo cha TFF Mnyanjani Tanga, umeamsha morali ya kupambana kwa wachezaji.

Akizungumza na Mwanaspoti baada ya mchezo huo, Mingange alisifu wachezaji wa timu hiyo kwa kufuata maelekezo yake vizuri, huku akiweka wazi bado ana kazi kubwa ya kufanya hasa ya kuboresha maeneo mbalimbali ili kutengeneza balansi kikosini.

“Mchezo ulikuwa ni mgumu sana lakini nimefurahia ari ambayo vijana wangu waliionyesha kuanzia mwanzoni hadi mwishoni mwa mechi yetu, kama nilivyosema tangu hapo awali bado tuko kwenye nafasi nzuri ya kusogea juu hivyo, acha tuone,” alisema.

Mingange aliongeza, ushindi huo ni moja ya jambo kubwa kwao kwani kwa sasa wanachokiangalia ni kupata pointi tatu bila ya kujali wamecheza soka la aina gani, kwa sababu lengo wanaloliangalia ni kuhakikisha timu hiyo inapanda Ligi Kuu Bara.

Kocha huyo aliyezifundisha timu mbalimbali za Ndanda FC, Mbeya City na Tanzania Prisons, tayari ameshakiongoza kikosi hicho katika michezo tisa hadi sasa na kati ya hiyo ameshinda sita na kupoteza mitatu akiwa nafasi ya nne na pointi 18.

Related Posts