Walalama bonde la kilimo kugeuzwa machimbo ya mchanga

Unguja. Wakazi wa Bonde la Donge Jangwani, Mkoa wa Kaskazini Unguja, wamelalamika kupokonywa mashamba yao waliokuwa wakiyatumia kwa kilimo badala yake yanachimbwa mchanga.

Kwa nyakati tofauti wamesema wanaishi maisha magumu kutokana na kukosa maeneo ya kuendeleza shughuli zao za uzalishaji mali.

Hata hivyo, wakati  wakieleza athari wanazopata kwa kukosa eneo la kulima baada ya maeneo yao kuchimbwa, Serikali imedai hakuna mkulima hata mmoja aliyeathirika.

Wakizungumza na Mwananchi katika eneo hilo jana Jumamosi Novemba 16, 2024 baadhi ya wakulima waliothiriwa na uchimbaji wa mchanga katika maeneo yao, wamedai wamechukuliwa ardhi yao na walikuwa wakiitumia tangu Mapinduzi matukufu ya Zanzibar mwaka 1964.

Yussuf Omar Juma amesema kwasasa maeneo yao wamepewa watu wengine na kuanzisha shughuli za uchimbaji mchanga wao wakibaki wasijue cha kufanya.

Amesema mashamba hayo ndio tegemezi kwao kwa kuwa wanafanya shughuli za kilimo kujikimu na maisha yao lakini kwa sasa mashamba hayo yamechimbwa mchanga na hayafai tena kwa kilimo.

“Serikali inatuhimiza wananchi kuilinda ardhi kwa lengo la kudumisha mazingira, kubaki salama ila kwa bahati mbaya sana kipindi hiki mtu anayekata mti amekuwa bora kuliko anayeilinda ardhi, hivyo kilio chetu bado tunakirudisha kwa Serikali ichukue hatua kuhusu wanaofanya hivi,” amesema Juma.

Amesema wakulima wanaotumia bonde hilo hawana ajira kwa sasa na mashamba hayo ndio kitega uchumi chao, ndio maana wanaiomba Serikali kuwasaidia.

Mkulima mwingine, Mzee Yussuf amesema kawaida ya wananchi wa kijiji wakishaambiwa kuwa jambo linafanywa na Serikali wanakosa nguvu ya kufuatilia.

“Wananchi wa vijijini wakishaambiwa jambo limetendwa na Serikali hawana uhuru wa kufuatilia, kilichobaki ni kushukuru Mungu na kukaa kimya ilihali wanaumia,” amesema Juma.

Bonde la Donge Jangwani linalolalamikiwa na wananchi kuchimbwa mchanga katika maeneo yao ya kilimo. Picha na Zuleikha Fatawi

Amesema Serikali ilitoa agizo kwa watu wanaomiliki mashamba na yanahitaji kuchimbwa mchanga waende kujaza mkataba, asilimia 70 itakwenda kwa Serikali na asilimia 30 itabaki kwa mmiliki.

Katika utaratibu uliowekwa na Serikali, mwananchi anayetaka kununua mchanga anaomba serikalini kupitia mfumo maalumu na tani moja inalipiwa Sh10,000.

Juma amesema kauli hiyo ndio inayotumiwa na watu wachache kujinufaisha wao bila kuzingatia utaratibu na kumuumiza mkulima mwenye eneo lake.

Solo Shija Luhende, amesema shamba lake ni miongoni mwa yaliothiriwa kwa kuchimbwa mchanga likiwa na viazi.

Pia, amesema hajui wakati wa mavuno watapitisha wapi mazao hayo kuyatoa shambani na kuyapeleka barabara kuu kwa kuwa hakuna gari inayoweza kufika shambani.

“Wakati wa mavuno tutalazimika kubeba mabegani kutoa mazao shambani na kupeleka juu ili kuchukuliwa na gari kupeleka barabara kuu,” amesema Luhende.

Amesema, awali walikuwa wanalipia Sh5,000 kutoa mazao yao shambani hadi kufikishiwa barabarani ila kwa sasa hivi ni ngumu kwani njia waliyokuwa wanaitumia imechimbwa mchanga.

Mwingine, Yussuf Kassim Iddi amesema eneo hilo limeharibiwa bila ya utaratibu maalumu, kwa mujibu wa sheria maeneo yanayotumika kwa kilimo hayaruhusiwi kuchimbwa mchanga.

Iddi amesema shamba hilo lilikuwa linalimwa mpunga, matikiti, mahindi, viazi na matango kwa ajili ya biashara kwa kuwa hiyo ndio ajira yao.

Mkulima huyo amesema shamba hilo limechimbwa mchanga bila ya kushirikishwa wananchi wanaolima eneo hilo.

“Hili shamba hatuwezi kusema kuwa linachimbwa na Serikali kwa sababu hawakuja kutuweka kikao tukazungumza na tukakubaliana, ndio maana tunaiomba Serikali imchukulie hatua huyo aliyefanya hivyo,” amesema Iddi.

Sambamba na hilo alitoa rai kwa wahusika wanaotoa vibali vya kuchimba mchanga kufanya tathimini ili kuona maeneo yanayopaswa kuchimbwa mchanga bila kuathiri kilimo na makazi ya watu.

“Wanaochimba mchanga hawazingatii mazingira na wanachimba kiholela bila kuwa na utaratibu maalumu, hivyo wafanye tathimini kwani wanaoathirika ni wakulima,” amesema Iddi.

Sheha wa Donge Mbiji, Zahor Abdalla Mzee  amekiri kuwepo kwa malalamiko hayo ya wakulima katika eneo hilo na tayari jambo hilo limeshafikishwa serikalini kwa hatua zaidi.

Takribani miezi minne tangu mashamba hayo yaanze kuchimbwa mchanga maeneo hayo bila ya utaratibu maalumu, imesababisha kukosa ajira na wengine kukata tamaa na maisha.

Mwananchi lilipomtafuta mtu anayedaiwa kuendesha shamba hilo katika shughuli za uchimbaji, Othman Ame amesema eneo hilo linachimbwa mchanga na Serikali na sio yeye kwa kuwa, hakuna raia yeyote anayechimbisha shimo la mchanga isipokuwa ni Serikali yenyewe.

Amesema, Serikali ndio inaruhusu eneo kuchimbwa mchanga baada ya kamati kujiridhisha.

“Hakuna sehemu nayoweza kuchimba shimo la mchanga kama Serikali haijui, hivyo shimo linafunguliwa (linachimbwa) baada ya Serikali kujiridhisha, inatangaza katika vyomba vya habari eneo lililoruhusiwa  kuchimbwa mchanga,” alisema.

Lori la mchaga likiwa linatoka kuchukua rasimali hiyo katika Bonde la Donge Jangwani eneo linalolamikiwa na wananchi kubadilishwa matumizi na kukosa eneo la kuendeshea shghuli zao za kilimo bila kushirikishwa Mkoa wa Kaskazini Unguja. Picha na Zuleikha FatawI

Hivyo, amelekeza iwapo kuna hoja yoyote inayohusiana na uchimbaji wa mchanga katika shimo hilo iulizwe Serikali ndio yenye majibu sahihi.

Amesema, “eneo linalotaka kuchimbwa mchanga kabla ya kuchimba ni lazima uiandikie barua wizara husika kwa lengo la kuja kuangalia eneo lililoombewa liko sahihi au halipo sahihi.”

Ame  amesema baada wizara kujiridhisha wanaandikiana mkataba maalumu, inatokea sintofahamu mhusika mkuu ni Serikali.

Hata hivyo, amesema tayari Serikali imeshafika kuanzia mkuu wa wilaya hadi wizara husika ili kumaliza jambo hilo na tayari imeshaagiza lifungwe.

Hata hivyo, licha ya shimo hilo kudaiwa kufungwa kwa wiki sasa mwandishi wa habari hii ameshuhudia uchimbaji mchanga wa eneo hilo bado ukiendelea.

“Hao ni wakulima wanasema tu hayo maneno ila hilo shamba limeshauzwa na mmiliki na siwezi kuongelea hilo nendeni wizarani mkachukue taarifa zote, mimi sina taarifa zaidi,” amesema mwekezaji huyo.

Mkuu wa Wilaya Kaskazini B Unguja, Hamid Seif Said ambaye ametajwa na wananchi hao kufika katika eneo hilo na kuahidi kughulikiaa tatizo hilo, amesema kwa sasa yupo likizo na kama kuna kitu chochote kinachohusu wilaya hiyo atafutwe mkuu wa Wilaya Kaskazini A Unguja anayekaimu nafasi yake.

Hata hivyo, alipotafutwa Kaimu mkuu wa wilaya hiyo, Othman Ali Maulid amesema hawezi kutoa majibu kwa sasa kwa kuwa hajafika katika eneo na kushuhudia.

“Unajua mimi ni DC wa Kaskazini A, nimekaimu maana mwenyewe yupo likizo na sijaanza rasmi, hivyo subiria niende site (eneo husika) nitakutafuta kutoa ufafanuzi,” amesema Ame.

Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Shaame Khamis Shamata alipoulizwa na Mwananchi kuhusu sakata hilo, amesema hana taarifa nalo ila dhamana hiyo ipo kwa wizara nyingine.

Hata hivyo, ameahidi watalifuatilia katika ngazi husika na kuangaliwa ikiwa kuna taratibu zimekiukwa na kuhakikisha haki za wananchi zinapatikana.

Mwananchi ilimtafuta Waziri wa Maji Nishati na Madini, Shaibu Hassan Kaduara amesema wachimbaji walitaka kuingia katika eneo la kilimo lakini hawakuwahi kuingia na uchimbaji mchanga umesitishwa.

“Tumeshachukua hatua ya kusitisha uchimbaji mchanga, wachimbaji waliingia kidogo ila wananchi walivyosema bado wanaendelea kulima tumesitisha,” amesema Kaduara.

Wakati wananchi wakisema wameathiriwa, Waziri anadai hakuna mwananchi yeyote aliyeathirika katika eneo hilo na maeneo yote yanayochimbwa mchanga ni tambarare sio milima.

Related Posts