Aussems ampa ujanja Guede | Mwanaspoti

KOCHA wa Singida Black Stars, Patrick Aussems, amesisitiza kuwa kila mchezaji ana nafasi sawa ya kuonyesha uwezo na kinachohitajika ni kila mmoja kutumia ipasavyo dakika anazopewa.

Aussems ametoa kauli hiyo kufuatia mjadala ulioibuka kuhusu kutotumika mara kwa mara kwa baadhi ya wachezaji akiwemo aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Joseph Guede katika kikosi cha kwanza, huku akionekana kutumika zaidi Elvis Rupia.

“Tunazingatia juhudi za kila mchezaji mazoezini na katika mechi. Kila mmoja atapata nafasi kulingana na mipango ya mchezo husika. Ninachoangalia ni mchezaji kufanya kazi yake ipasavyo na kuonyesha thamani yake uwanjani,” alisema Aussems. 

Rupia kwa sasa ndiye kinara wa mabao wa timu hiyo akiwa amefunga matatu Ligi Kuu Bara, huku Guede hajapata bao.

Hata hivyo, kipindi cha kalenda ya Fifa kimeleta matumaini kwa Guede baada ya kufunga bao katika ushindi wa 3-1 wa Singida dhidi ya Fountain Gate kwenye mechi ya kirafiki. Rupia aliongeza mengine mawili. 

Aussems anatarajia kuona ushindani zaidi kutoka kwa washambuliaji wake, hasa wakati Singida Black Stars inapojiandaa kwa ratiba ngumu ya mechi tatu ndani ya siku nane mara baada ya kalenda ya FIFA. Mechi hizo ni dhidi ya Tabora United (ugenini), Azam FC (ugenini), na Simba SC (nyumbani). 

“Ratiba yetu ni ngumu, lakini nina imani na wachezaji wangu. Ushindani ndani ya timu ni muhimu, na hiyo inanipa uhakika kwamba tutakabiliana vyema na changamoto zinazokuja,” aliongeza Aussems. 

Singida Black Stars ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 23, nyuma ya Yanga ambayo ipo nafasi ya pili na pointi 24, Simba ndio vinara wa ligi hiyo wakiwa na pointi 25.

Related Posts