Chalamila: Nipo tayari kuwajibika kama sikutimiza wajibu tukio la Kariakoo

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema yupo tayari kuwajibika, endapo ofisi ya Waziri Mkuu itafanya uchunguzi na kujiridhisha kwamba yeye na timu yake hawakuwajibika ipasavyo katika uokozi kwenye ajali ya jengo la ghorofa lililoporomoka katika soko la Kariakoo.

Jengo hilo liliporomoka Juzi na kusababisha vifo na majeruhi.

Akizungumza wakati wa tukio la kuaga miili ya watu 15 waliopoteza maisha katika ajali hiyo, Chalamila amesema yeye na timu yake wanahisi wamefanya kazi ya uokozi hadi pale walipofika.

“Mpaka sasa tunaendelea na zoezi la uokozi, hata hivyo baada ya jengo kuporomoka, ilitulazimu kuamua lisibomolewe na kutumia akili ya uokozi,” amesema Chalamila mbele ya Waziri Mkuu anayeongoza tukio la kuaga miili ya waliopoteza maisha.

Ameongeza kuwa “Kuna watu wengi waliona hatujawajibika ipasavyo, niombe pale utakapobaini hatukuwajibika, nitakuwa tayari kuwajibika”

Amesema, Ofisi ya Waziri Mkuu ina taarifa pana na inafahamu mambo mengi, hivyo itakapojiridhisha hakuwajibika na timu yake yupo tayari kuwajibika.

Chalamila amesema hadi jana saa 6 mchana alikuwepo kijana dereva wa Uber, aliyekuwamo ndani ya jengo hilo na kuwapigia simu.

“Akiwa ndani ya jengo, alituambia nguvu zinamuishia yeye watu wengine na hivi ninavyozungumza tuliwaokoa na wote wako hospitali,” amesema

Amesema kuna watu wanahisi waliopoteza maisha wao kina Chalamila walichelewa kuwaokoa ndio maana wamefariki.

“Madaktari ni mashahidi, wengi walifariki baada ya tukio, wengi wao walipata majeraha ya kuangukiwa kuta na matofali

“Sisi ni wanadamu yawezekana kuna watu nimewakwaza, naomba nirudie tena nitakuwa tayari kuwajibika,” amesema.

Chalamila alibainisha pia kuwepo usalama wa kutosha na hakuna mizigo itakayoibiwa kwenye jengo hilo.

Related Posts