DC SIMANJIRO AKABIDHI GARI JIPYA TAKUKURU MIRERANI

Na Mwandishi wetu, Mirerani

MKUU wa Wilaya ya Simanajiro Mkoani Manyara, Mwalimu Fakii Raphael Lulandala ameikabidhi gari jipya Taaasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kituo cha Mirerani.

DC Lulandala amekabidhi gari hilo ndani ya ukuta unaozunguka machimbo ya madini ya Tanzanite Mirerani kwa mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Simanjiro, Adam Mbwana na kuiagiza taasisi hiyo kutumia gari hilo kwa malengo kusudiwa.

Amesema kijiografia wilaya ya Simanjiro ina eneo kubwa la utawala hivyo kwa kupatikana kwa gari hilo kutasababisha utendaji kazi kuwa bora zaidi katika Tarafa ya Moipo.

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa gari hili kwa ajili ya matumizi ya taasisi ya TAKUKURU ukanda huu wa Tarafa ya Moipo kwenye suala la usafiri,” amesema DC Lulandala.

Amesema kupitia gari hilo watumishi wa TAKUKURU wataweza kufika maeneo mbalimbali ya kata za Mirerani, Endiamtu, Naisinyai na Shambarai na kutoa elimu juu ya rushwa.

“Hapa Simanjiro nina taasisi ya TAKUKURU inayohudumu Wilaya ya Simanjiro yenye makao makuu yake mji mdogo wa Orkesumet na TAKUKURU iliyopo Tarafa ya Moipo ambayo ndiyo imepata gari,” amesema DC Lulandala.

Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Simanjiro Adam Mbwana ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia gari hilo.

Mbwana amesema kupitia gari hilo TAKUKURU Mirerani watafanya kazi zao zaidi kwa urahisi zaidi tofauti na awali ambapo kituo hicho hakikuwa na usafiri wa kuifuata jamii.

Mkuu wa TAKUKURU Mirerani, Sultan Ng’aladzi amesema kupitia gari hilo watakuwa na kitendea kazi kizuri cha kufanya kazi katika maeneo ya Tarafa ya Moipo.

“Hivi sasa hata kutoa elimu ya TAKUKURU Rafiki itakuwa rahisi kwani maeneo ya Kilombero au Lengasiti tutaweza kufika na kutoa somo mbalimbali ya kupinga rushwa,” amesema.

 

Related Posts