KOCHA wa Simba, Fadlu Davids amesema kurejeshwa katika ratiba kwa pambano la Ligi Kuu Bara dhidi ya Pamba FC Novemba 22 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza imekaa poa kwani itampa taswira nzuri kabla ya kukutana na Bravos do Maquis ya Angola katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Fadlu alisema mchezo huo wa ushindani utakuwa mzuri kwao wa kutengeneza fitinesi na kuendana na ushindani kwa baadhi ya wachezaji ambao hawakupata nafasi ya kucheza timu za taifa, katika kipindi hiki cha michezo mbalimbali ya kufuzu Afcon.
“Tumecheza na KMC mchezo wa kwanza wa kirafiki ambao umekuwa na matokeo chanya kwetu ingawa hatuwezi kuuweka katika levo za kiushindani, Pamba itatusaidia japo tunapaswa kuendelea kushikilia hapa tulipo ili itupe morali ya mechi inayofuata.”
Kocha huyo aliongeza katika michezo miwili ijayo wanapaswa kupambana na kuendelea kuonyesha ubora ambao wamekuwa nao kwa mechi za hivi karibuni, huku akitoa tahadhari kwa nyota wa kikosi hicho kuacha kufikiria kwanza mechi dhidi ya FC Bravos.
“Baada ya kutokuwa na uhakika wa mchezo wetu na Pamba kuchezwa, tayari akili za wengi wetu walishaanza kufikiria Bravos, jambo ambalo sio baya kwa sababu inaonyesha jinsi gani wako tayari kiakili, japo tunaenda mechi moja baada ya nyingine,” alisema kocha msaidizi huyo wa zamani wa Raja Casablanca ya Morocco.
Simba iliyopo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi 25, baada ya kucheza 10, imeshinda minane, sare mmoja na kupoteza mmoja, ikifunga mabao 21 na kuruhusu 3 itakutana na Pamba iliyoshinda mchezo mmoja tu kati ya 11 iliyocheza.
Baada ya hapo kikosi hicho kitarudi jijini Dar es Salaam kwa ya maandalizi ya kupambana na Bravos Novemba 27 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikiwa ni mchezo wa kwanza wa makundi ya Kombe la Shirikisho, Kundi A lenye timu nyingine za CS Constantine ya Algeria na CS Sfaxien ya Tunisia.