Hatari iliyopo Kariakoo ubomoaji, ujenzi wa majengo

Dar es Salaam. Ubomoaji holela usiofuata sheria ni hatari nyingine ya kiusalama na kiafya inayowakabili wananchi wanaofanya shughuli zao au kwenda katika eneo la Kariakoo, Dar es Salaam. Uchunguzi wa Mwananchi umebaini.

Katikati ya maandalizi ya habari hii ya uchunguzi wa takribani miezi mitatu ikiangazia ubomoaji wa majengo kwenye eneo hilo ambalo ni kitovu cha biashara nchini, Jumamosi ya Novemba 16, 2024 jengo la ghorofa nne katika Mtaa wa Kongo na Mchikichi liliporomoka na kusababisha vifo vya watu 16, majeruhi 86 na uharibifu wa mali za mamilioni ya fedha.

Jengo la shirika la nyumba la Taifa lilikuwa linabomolewa Septemba 2, 2024 katika mtaa wa Congo na Tandamti

Uchunguzi huo wa Mwananchi uliofanyika kati ya Juni – Oktoba 2024 umebaini shughuli za ubomoaji zimekuwa zikifanyika pasipo kuchukuliwa kwa tahadhari.

Hakuna hata jengo moja kati ya yaliyofanyiwa uchunguzi lililokidhi vigezo vya ubomoaji kwa asilimia 100 jambo ambalo sio tu, ni kinyume cha sheria na taratibu, bali hatari kwa maisha ya watu wanaofanya kazi na kupita yalipo majengo hayo.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, ubomoaji huo unaendeshwa kinyume na Kifungu cha 55 cha Sheria ya Usalama na Afya Kazini ya mwaka 2003, kinachotamka ni haki ya wafanyakazi na umma kupata mazingira salama na kila mwajiri au mmiliki wa eneo la kazi anapaswa kuhakikisha usalama na afya ya wafanyakazi wake na watu wote walioko karibu na eneo hilo.

Juni 25, 2024 jengo hili lilibomolewa Mtaa wa Raha na hakukuwa na tahadhari yoyote.

Si hiyo tu, hauzingatii Kifungu cha 47 cha Sheria ya Mipango Miji ya mwaka 2007, ambacho kinasema utekelezaji wa shughuli za kubomoa majengo lazima uzingatie mipango miji na usalama wa raia kama zinavyobainishwa na Katibu wa Chama cha Usalama na Afya Mahala pa Kazi (Tohasa), Abdulkadir Mwinyi anasema ni pamoja na kuwapo muda wote kwa mtaalamu wa usalama na afya kazini anayesimamia mradi husika ambaye ambaye ataajiriwa na kampuni husika.

“Mtu huyu anatakiwa kuwepo katika ufuatiliaji wa yale yote ambayo yameorodheshwa na mtekeleza mradi ambayo yameandikwa katika nyaraka wakati wa kuomba kibali cha ubomoaji,” anasema.

Anasema msimamizi huyo anatakiwa kuwapo katika eneo la kazi asubuhi kuhakikisha wafanyakazi wana vifaa muhimu kwa ajili ya usalama wao kabla ya kuruhusiwa kuendelea na kazi.

Jambo jingine linalopaswa kuzingatiwa ni mafunzo kwa zile kazi zinazofanyika kwenye eneo jambo ambalo anasema halifanyiki kwa baadhi ya miradi.

Ujenzi ukiendelea na chini wafanyabiashara wanaendelea kufanyabiashara zao katika mtaa wa Sikukuu

Wanaozingatiwa katika hilo la usalama na afya za watu, Mwinyi anasema si wafanyakazi pekee, “wapo wenye majengo wanaoingia katika maeneo ya ujenzi bila kujali usalama wao na msimamizi haoni umuhimu wa kuwapatia elimu kwa sababu ni mwenye mradi.

“Unakuta mwenye mradi anakuja na mtoto wake kutembelea eneo lao bila kujali umuhimu wa kuvaa vikinga hatari, ikitokea kitu kimetokea juu ni hatari kwa mtoto.”

Jingine muhimu lililobainika kukiukwa ni wapita njia na wafanyabiashara wadogo kukosa ulinzi wa kutosha kwa kutokuwapo kwa mipaka ya usalama na vumbi lisilodhibitiwa.

Mkazi wa Kariakoo, Fatuma Abdallah anasema japo yeye si mjuzi wa masuala ya ujenzi, anaamini baadhi ya miradi ya ujenzi na ubomoaji inakiuka taratibu za kiusalama akifafanua anasema sehemu kubwa anayopita kwenye maeneo ya ujenzi hakuna alama za tahadhari wala vizuizi vya kutosha.

Fatuma anasema aliwahi kushuhudia mtoto akikoswakoswa na jiwe walipokuwa jirani na eneo ambalo linabomolewa kutokana na kutokuwapo tahadhari yoyote.

Jengo la Shirika la Nyumba la Taifa la Mtaa wa Tandamti likiwa linabomolewa Julai 26, 2024.

Mteja anayefika Kariakoo mara kwa mara kununua bidhaa, Hamisi Maneno anasema, “mara nyingi ninapita kununua bidhaa na nimeshuhudia ujenzi au ubomoaji ukiendelea bila tahadhari. Hii ni hatari sana, hasa kwa wapita njia.”

Mchuuzi wa magauni katika Mtaa wa Raha, Kariakoo, Fatma Hassan anasema wakati mwingine ubomoaji unafanywa bila hata kuwajulisha wanaofanya biashara jirani na jingo husika.

“Tulisikia ghorofa lililopo litabomolewa lakini hatukuambiwa lini. Siku moja tulipokuwa tunaendelea na shughuli zetu tulishangaa kuona watu wakigonga huko juu na tulikuwa tunarukiwa na vikokoto na vumbi,” anasema Fatma na kuongeza;

“Siku moja, wakati nikiwa na wateja, kifusi kilianguka karibu na meza yangu ilikuwa ni hatari. Hatuwezi kufanya biashara kwa amani katika mazingira kama haya.”

Fatma anasema ubomoaji haufuati sheria za usalama kwani vitu vinafanywa harakaharaka bila kujali athari kwa wafanyabiashara na wapita njia na hawajui taarifa za ukiukwaji huo wa sheria wanauripoti kwa nani kwani japo anasema baadhi ya taarifa zilizowahi kutolewa mtandaoni zilifanyiwa kazi kwa kiwango kidogo.

Kilio cha mafundi na vibarua

Ukiukwaji huo wa sheria ni kilio pia cha mafundi na vibarua wanaohusika na ujenzi na ubomoaji wa majengo Kariakoo wengi wakilalamikia ukosefu wa vifaa muhimu vya usalama kama vile kofia ngumu, miwani ya kujikinga na vumbi na mavazi ya kinga hivyo kuwa katika hatari ya kuumia na hata kupoteza maisha.

“Mara nyingi tunaingia kwenye maeneo ya kazi bila kupewa maelekezo ya kutosha au vifaa vya kujikinga. Tunatakiwa kufanya kazi kwenye majengo yaliyo hatarini kubomoka na yaliyowekewa malengo ya kubomolewa lakini hawatupatii vifaa kama sheria zinavyoagiza,” anasema kibarua, Maneno Omary.

“Kazi hii ni ngumu na hatari, lakini tunalazimika kufanya kwa sababu ya tunahitaji wa kipato.”

Wakati maneno akisema hayo, mwenzake Zablon Solomon anasema,”Serikali inatakiwa kusimamia vizuri hizi kazi za ubomoaji. Zinafanywa kwa haraka na wasimamizi hawazingatii kabisa usalama wetu. Kuna ajali nyingi ambazo zinaweza kuepukika kukiwa na usimamizi mzuri na kufuata sheria za ujenzi.”

Fundi Hamidu Kiandae anasema kazi ya ubomoaji si rahisi kama watu wengine wanavyofikiria, “watu wanadhani kazi ya ubomoaji ni rahisi, lakini ni hatari sana… tunatumia nguvu nyingi kwa sababu ya nyundo na hakuna vifaa maalumu na wakati mwingine hakuna hata mkandarasi au mtaalamu wa usalama anayefuatilia. Tunajitahidi kuwa makini, lakini hatuwezi kuzuia ajali zote bila msaada wa vifaa na sheria kufuatwa.”

Dereva wa moja ya mashine ya ubomoaji, Hassan Leo anasema, “nipo hapa kwa ajili ya kubomoa baadhi ya sehemu na unaona wafanyaji kazi hawana vifaa muhimu. Wanatakiwa kutoa hizo nondo hata linapofika gari la kukusanya kifusi ni vumbi tupu na watu hawajali lolote.”

Mkandarasi anayesimamia miradi kadhaa ya ujenzi Kariakoo ambaye hakutaka jina lake liandikwe anasema wengi wanashinikizwa kukamilisha miradi haraka bila kuzingatia sheria na kanuni zinazolinda usalama wa wafanyakazi na wapita njia.

“Miradi mingi inafanywa haraka kutokana na shinikizo la wamiliki wa majengo ambao wanataka kazi ifanyike haraka ili waingie kwenye biashara mapema. Hii inasababisha baadhi ya sheria za usalama kupuuzwa,” anasema.

Kwenye ubomoaji wa majengo anasema, sheria zinataka kufanyika kwa tathmini ya awali kwenye miundombinu ya jengo kabla ya ubomoaji kuanza lakini, “tathmini hii mara nyingi inapuuzwa jambo ambalo linaweza kusababisha maafa kwa majengo jirani au hata ajali kubwa.”

Anasema wataalamu kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira na Usalama Mahala pa Kazi (Osha) wanahusika moja kwa moja katika kufanya ukaguzi wa maeneo ya ujenzi.

Hata hivyo, mkandarasi huyo anasema, “si miradi yote hao watu wa Osha wanapita, ninaweza kusema kama eneo hili ukifuatilia hakuna mtu atakayesema amepita au kupewa uthibitisho wao kuwa wamefanya ukaguzi. Kinachozingatiwa ni kibali cha ubomoaji na ujenzi mengine ni funika kombe.”

Baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Osha, Hadija Mwenda kutafutwa kwa wiki kadhaa bila mafanikio ili kutoa ufafanuzi wa madai hayo ya mhandisi msimamizi, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi aliwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za maeneo yenye vihatarishi vya usalama ili hatua zichukuliwe.

Kwa kauli hiyo, Naibu waziri huyo alimwagiza bosi wa Osha kufanya ukaguzi katika maeneo yote ambayo wananchi wanayalalamikia na hata yale ambayo hakuna malalamiko lakini yana viashiria vya hatari.

Anasema ikiwa wahandisi na makandarasi hawatazingatia sheria, kuna uwezekano wa majengo wanayobomoa kuporomoka au watu kujeruhiwa vibaya, kwani kuna wakati wanaona watu wakidondokewa na mawe lakini pia wapo wanaoingia ndani ya ujenzi bila tahadhari.

Maelezo ya mhandisi wa Jiji

Lakini majibu ya Mhandisi wa Jiji la Dar es Salaam, Lusekelo Mwakyami yanakinzana na madai hayo kwani anasema ukaguzi unafanyika na wanapobaini ukiukwaji wa sheria huchukua hatua ikiwamo kusimamisha ubomoaji au ujenzi.

Anasema utaratibu uliopo kwa eneo la Kariakoo ni kwamba ubomoaji unafanyika usiku na ili kuondoa hatari zote hushirikiana na sekta nyingine wakiwamo Shirika la Umeme la Tanzania (Tanesco), Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Anasema wanapogundua kuwapo kwa kasoro, anayewajibika ni mmiliki, “kasoro zote zinazojitokeza zinakuwa za mwenye jengo, mhandisi ni msimamizi hivyo ni ngumu kumuadhibu kwa sababu si mhusika.”

Hata hivyo, anachokieleza mhandisi juu ya ubomoaji kufanyika usiku kwani Mwananchi lilishuhudia ubomoaji huo ulifanyia mchana huku wananchi wakipita maeneo hayo na hakukuwa na tahadhari yoyote iliyowekwa.

Tayari Rais Samia Suluhu Hassan amemtaka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuchunguza majengo na ujenzi wote unaoendelea Kariakoo.

Majaliwa naye ametangaza timu ya watu 19 ikiongozwa na Brigedia Jenerali Hosea Ndagala,Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu. 

Usikose sehemu ya pili ya stori hii

Related Posts