Maduka jirani na ghorofa lililoporomoka yazuiwa kufunguliwa

Dar es Salaam. Wakati shughuli za uokozi wa jengo la ghorofa kuporomoka zikiingia siku ya tatu leo Jumatatu, Novemba 18, 2024, maduka yaliyo eneo la Msimbazi na yale ya Mchikichini, Kariakoo jirani na jengo hilo yamezuiwa kuendelea na biashara.

Mbali na maduka, usafiri wa umma yakiwamo mabasi ya mwendokasi yanayokwenda Gerezani yanaishia Kituo cha Fire.

Mabasi hayo yamelazimika kuishia Kituo cha Fire na kugeuza, huku daladala zikiishia kituo cha mabasi cha Msimbazi yalipo maduka ya vipodozi.

Askari wa Jiji, Zimamoto na Uokoaji, wanajeshi wapo eneo la tukio kuendelea na shughuli mbalimbali za uokozi na wengine kuzuia vyombo vya moto kukatisha eneo hilo.

Kumefungwa utepe kuanzia jirani na kituo cha mafuta cha Big Bon na kuzuia watu kuvuka kuelekea yalipo mataa ya Gerezani na watembea kwa miguu kuelekezwa upande mwingine wa kupita.

Maduka ya eneo hilo kuelekea upande yalipo mataa ya Uhuru na Msimbazi na jirani na ghorofa lililoporomoka yote yamefungwa.

Maduka ya jirani na ghorofa lililoporomoka yakiwa yamefungwa leo Jumatatu Novemba 18, 2024.

Baadhi ya wauzaji wameeleza kuzuiwa kufungua maduka hayo.

“Nimefika kwa ajili ya kufanya kazi, nikaambiwa haturuhusiwi kufungua,” amesema Zainab Idd.

Muuzaji mwingine, Edson Edmund amesema analazimika kurudi nyumbani baada ya kuzuiwa kufungua duka.

“Ndio tunasubiri utaratibu mpya watakaotuambia, lakini kwa leo tumeambiwa ni marufuku kufungua,” amesema.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Seleman Jafo aliyekuwa eneo la tukio amesema, watahakikisha mali za watu zinakuwa salama.

“Uokozi unaendelea, tunashukuru Watanzania wametoa ushirikiano mkubwa hadi sasa, hatutasimama hadi kumfikia mtu wa mwisho, lakini pia tutahakisha mali za watu zinakuwa salama,” amesema.

Shughuli za uokozi zinaendelea huku hadi kufikia jana Jumapili, saa 4 asubuhi vifo vilikuwa vimefikia 13 na wengine 84 walipata majeruhi huku 26 wakiwa bado wako hospitalini wakiendelea na matibabu.

Endelea kufuatilia Mwananchi

Related Posts