Dar es Salaam. Majeneza 15 yenye miili ya watu waliopoteza maisha katika ajali ya ghorofa lililoporomoka kwenye soko la Kariakoo yamewasili viwanja vya Mnazi mmoja tayari kuanza tukio la kuagwa.
Majeneza yenye miili hiyo yaliwasili saa 7:34 mchana viwanjani hapo na kuweka eneo maalumu lililoandaliwa ikiwa ni dakika saba baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwasili uwanjani hapo saa 7:27 mchana.
Miili hiyo iliwasili ikiwa kwenye magari kadhaa ya jeshi ikiongozwa na king’ora cha gari ya wagonjwa.
Ilipowasili, ilibebwa na wanajeshi kwa paredi maalumu na kwenda kuiweka eneo lililoandaliwa ambalo kwenye kila meza iliyobeba jeneza kuliwekwa kiti kimoja, hivyo kufanya idadi ya viti kuwa 15.
Wakati miili hiyo ikiingizwa uwanjani hapo, ndugu na jamaa wa marehemu na waombolezaji wengine walikuwa wakiangua vilio.
Uwanjani hapa, Askari wa Kutuliza Ghasia (FFU) wanaendelea kupokea na kuongoza familia na waombolezaji wengine, huku askari wa jiji (Mgambo) wakaendelea kutoa huduma ikiwamo maji ya kunywa kwa waombolezaji na watu wa msalaba mwekundu wakitoa msaada wa huduma ya kwanza kwa baadhi ya waombolezaji.
Tukio la kuaga miili hiyo inaongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.