Morogoro. Mama aliyezaa watoto 15, Neema Kenge (39) mkazi Mtaa wa Mgonahazeru Manispaa ya Morogoro, amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Baba wa watoto hao, Simon Thomas (55) ameiomba Serikali kumsaidia malezi kwa kuwapatia mahitaji muhimu watoto wanne kati ya hao, ambao wanasoma shule ya msingi.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu Novemba 18, Thomas anayefanya kazi ya ulinzi, amesema mkewe alikuwa akimsaidia malezi kwa kuwa alikuwa akifanya biashara ndogondogo za genge na mkaa.
Hivyo, ameiomba Serikali kumuingiza kwenye ruzuku ya mpango wa kunusuru kaya maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), ambayo alikuwa akipata marehemu mkewe, ili imsaidie kupata mahitaji ya watoto wake pamoja na chakula.
“Hapa nilipo nimevurugwa kwelikweli mwenzangu alikuwa msaada mkubwa kwenye kutunza familia hii, mimi nikienda kutafuta riziki, mwenzangu anabaki hapa nyumbani anaangalia watoto, sasa nimebaki peke yangu na sina pa kuwapeleka maana kikosi hicho chote nani atakayekubali kunilelea,” amesema Thomas.
Hivyo, amewaomba wasamaria wema kumtafutia kazi mtoto wake mkubwa wa kiume ambaye amemaliza kidato cha nne ili amsaidie kuwalea wadogo zake.
Amesema mwanaye huyo amesoma kwa ufadhili wa kituo kimoja cha kulelea watoto kilichopo Kibaha, mkoani Pwani. “Huyu kijana wangu ni wa pekee aliyefanikiwa kufika elimu ya sekondari, nawaomba Watanzania na hasa majeshi yaweze kumpa kazi, anisaidie kuwalea wadogo zake maana katika watoto wangu 15, wapo mabinti watatu wamezalishwa na wanaume wasiojulikana na wapo hapa nawalea wao na hao wajukuu.”
Ameongeza kuwa; “Huyu Binti yangu mkubwa mwenye miaka 18 kwa sasa ndiye ninayemtegemea atunze wadogo zake, ndugu ninao lakini ndio maisha yamekuwa magumu sio rahisi akutunzie watoto wote hawa.”
Akizungumzia kwa sharti la kutopigwa picha, mtoto huyo aliyejitambulisha kwa jina la Thomas Simon (19), anasema mbali ya kuhitimu kidato cha nne, lakini pia amejifunza kazi mbalimbali za mikono kama kilimo cha bustani na mpira.
“Awali mimi na ndugu zangu watatu, dada zangu wawili na kaka yangu tulichukuliwa na kwenda kuishi kwenye kituo kilichonisaidia kunisomesha, lakini wenzangu wote walishindwa kuendelea na masomo na hata kuishi kituoni hapo wakarudi nyumbani, mimi nikavumilia na mpaka sasa bado niko mikononi mwa kituo hicho,” amesema Thomas.
Hata hivyo amekiri kuwa hakuwa na ufaulu mzuri wa kidato cha nne ambao ungemuwezesha kuendelea na masomo ya kidato cha tano.
“Lakini nilishajaribu kuomba kazi maeneo tofauti mpaka kwenye majeshi, sijapata kwa sababu wazazi wangu pia hawakunitengenezea chetu cha kuzaliwa hivyo nikakosa nafasi ya jeshi,” amesema Thomas.
Kijana huyo anasema sababu mojawapo iliyochangia dada zake kubebeshwa mimba ni ugumu wa maisha.
Anasema muda mwingi walikuwa wakiutumia mtaani kusaka riziki na huko ndiko walikokumbana na wanaume waliowapa mimba na kutokomea.
“Kwa sasa wasiwasi wangu ni wadogo zangu wengine wa kike kama mama alikuwepo na alikuwa akipambana kuwalisha na akashindwa kuwalinda je, kwa sasa hawa wadogo usalama wao uko wapi, natamani watokee wasamaria wema na wamiliki wa vituo waje wawachukue hawa wadogo wakawalee,” amesema Thomas.
Ustawi wa jamii wazungumza
Akiizungumzia familia hiyo, Ofisa maendeleo ya jamii katika Kata ya Mbuyuni, Alicia Mbaga amesema baada ya maziko ya mama huyo, ofisi yake itakaa na wadau mbalimbali kuona namna ya kuisaidia familia hiyo.
“Kuna haja kubwa ya kuisaidia familia hii, tunaihakikishia usalama na watoto wanaosoma tutahakikisha wanaenda shule kama kawaida,” amesema.
Amekiri kuwa familia hiyo ni kubwa na inaishi katika mazingira magumu sana.
“Ni kweli hii familia ni kubwa na inaishi katika mazingira magumu sana, kula yao, vaa yao na hata sehemu ya kulala pia ni changamoto, hivyo tutakaa na kuangalia namna ya kuisaidia,” amesema.
Naye Diwani wa Mbuyuni, Samwel Msuya amesema familia hiyo awali ilikuwa ikipata ruzuku ya Tasaf, lakini baadaye ilitolewa kwenye ruzuku hiyo kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Hata hivyo, amesema analibeba hilo na atafanya mawasiliano na wataalamu wake kwenye kata waone namna nzuri ya kuiwezesha familia hiyo.
“Taratibu za Tasaf ni kwamba mnufaika anapewa ruzuku Kwa muda fulani Ili aweze kujikwamua na baadaye anapewa mtaji ili akajitegemee kwa kuanzisha biashara ,huyu mama alishapewa mtaji na muda wake wa kupewa ruzuku ulishaisha, isipokuwa tutaona namna ya kusaidia hii familia,” amesema diwani huyo.