LICHA ya kupoteza mchezo mmoja wa Ligi ya wanawake dhidi ya ndugu zao, JKT Queens, Mashujaa msimu huu imepania kufanya vizuri ikiwezekana kumaliza nafasi tatu za juu.
Mechi nne za ligi, Mashujaa imepoteza mchezo mmoja dhidi ya JKT mabao 2-0, sare mbili dhidi ya Yanga Princess 1-1, 0-0 na Get Program ikishinda 3-0 na Ceasiaa Queens.
Akizungumzia juu ya kikosi hicho, Koch Mkuu Greyson Haule alisema sio mwanzo mbaya kwao wakiitaka nafasi ya tatu kwenye msimamo.
Haule aliongeza kuwa kama timu wanapambana kuhakikisha kila mchezo wanapata pointi tatu na kujiweka salama kwenye malengo yao.
“Tumeanza na michezo mikubwa miwili dhidi ya JKT na Yanga na tunashukuru tuliondoka na pointi moja, malengo yetu ilikuwa kuchukua alama kwa kila mchezo,” alisema Haule.
Msimu uliopita timu hiyo kwenye mechi nne za mwanzo ilipata ushindi mchezo mmoja dhidi ya Alliance kwa mabao 4-1 ikipoteza tatu dhidi ya Simba Queens 3-2, JKT 10-0, Yanga 6-1 na 3-2 Simba Queens.