Dar es Salaam. Mvutano wa baadhi ya viongozi wa Chadema ukiwamo wa uchaguzi wa ndani, wa Serikali za mitaa, madai ya rushwa na kugawana madaraka na Chama cha Mapinduzi (CCM), ni miongoni mwa hoja zinazotarajiwa kuzungumzwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Kesho Jumanne, Novemba 19, 2024, Mbowe atakuwa na mkutano na waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya chama hicho Mikocheni, jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, swali linabaki, Mbowe anakuja na dawa ya minyukano inayoendelea ndani ya chama hicho baada ya kimya cha muda mrefu?
Taarifa ya mkutano wa Mbowe iliyotolewa na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema leo Jumatatu, Novemba 18, 2024, imekuja wakati ambao kiongozi huyo akiwa kwenye kimya cha zaidi ya miezi miwili licha ya mambo hayo kukigubika chama hicho.
Hata alipotafutwa mara kadhaa kwa simu na kwa ujumbe kupitia WhatsApp, Mbowe hakupokea wala kujibu ujumbe.
Mkutano wa Mbowe unakuja wakati kukiwa na kauli za kushutumiana hadharani miongoni mwa viongozi waandamizi wa chama hicho.
Fukuto katika chama hicho linazidi wakati kikiendelea na uchaguzi wa ndani, huku kikikabiliwa na uchaguzi wa Serikali za mitaa ambao wagombea wake wengi wameenguliwa sehemu mbalimbali nchini.
Si kuenguliwa tu, chama hicho kimeshindwa kusimamisha wagombea kwenye maeneo yote ya vijiji, vitongoji na mitaa, hata kabla ya kuenguliwa kwa sababu mbalimbali.
Katikati ya ukimya huo, wajumbe wenzake wa kamati kuu wamekuwa wakiibua tuhuma nzito dhidi ya chama hicho na kuibua mijadala juu ya mwelekeo wa chama hicho. Mbowe amekuwa kimya huku washindani kwenye siasa wakitumia nafasi hiyo kuwapiga vijembe.
Novemba 12, 2024, Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, Tundu Lissu aliitisha mkutano wa waandishi wa habari mjini Singida na kuwaeleza kutoridhishwa na mwelekeo wa uchaguzi wa Serikali za mitaa, akisema uchaguzi huo umekwisha na kwamba wanapaswa kujipanga upya.
Katika mkutano huo, Lissu alidai chama hicho kilidanganywa na CCM kwa lugha laini ya maridhiano.
“Tukaingiziwa vijineno vinavyosema hivi, msiwe wakali sana mtapewa Serikali ya nusu mkate,” alisema Lissu.
Hata hivyo, Chadema ilitoa taarifa kwa umma iliyosainiwa na Mrema ikikanusha hoja hizo, ikisema chama hicho hakijawahi kukubaliana na CCM kugawana madaraka.
Mbali na kauli hiyo, Lissu amekuwa akitoa kauli za madai ya kuwepo wa rushwa ndani ya chama hicho, akiwaonya makada kutojihusisha nayo.
Chadema pia inapitia kipindi kigumu cha uchaguzi wa ndani na baadhi ya maeneo zimezuka vurugu. Haya ni baadhi ya mambo ambayo Mbowe yanamsubiri kujua atayazungumziaje.
Novemba 16, 2024 Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema alimtaja Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Benson Kigaila, akisema alizembea alipokuwa akisimamia uchaguzi wa chama hicho mkoani Arusha Novemba 14, 2024 na kusababisha vurugu.
Lema aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, alidai kuwa, alilazimika kumuomba Kigaila ateremke akawazuie waliokuwa wanafanya fujo kwa kuwa mmoja wao ni rafiki yake mkubwa.
Lema alidai siku chache zilizopita, mwanachama mmoja akiwa na wenzake walifanya fujo kwenye uchaguzi wa Monduli mpaka uchaguzi ukaahirishwa.
“Mnaweza kusema kwa nini haya mambo msiongee kwenye vikao vya ndani, haya yataongelewa kwenye vikao vya ndani na lazima yaongelewe nje kwa sababu yameshaharibu taswira za watu, nimetukanwa na kudhalilishwa sana na haya maneno yako barabarani,” alidai.
Mbali na vurugu hizo, imepita miezi sita tangu uchaguzi wa kumpata mwenyekiti wa Mkoa wa Njombe uliowakutanisha Rose Mayemba na Ahadi Tweve ulipovunjika Mei 24, 2024.
Uchaguzi huo uliokuwa umerudiwa ulivunjika baada ya baadhi ya wanachama kudai baadhi ya wajumbe kutoka wilayani Makete hawakupaswa kushiriki kwa kuwa hawakuwa wajumbe halali na mpaka sasa uchaguzi huo haujarejewa.
Vurugu hizo zinakuja wakati Lissu kwa nyakati tofauti amenukuliwa akisema chama hicho kiliyumba na kuwachanganya wanachama.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda amesema ukimya huo ulizua sintofahamu katika chama.
“Ukimya wa mwenyekiti ni mzito ni sawa na kiza totoro katika kipindi ambacho tulitakiwa kuona muunganiko wa chama, yaani tuone viongozi wote wakiongea kauli moja.
“Sasa tunapoona wengine wanaongea tena wanakichimba chama na mwenyekiti yupo kimya, basi tujue kuna fukuto la ndani kwa ndani linalokifanya chama kisisimame kwa umoja,” amesema.
Dk Mbunda amesema, “hiyo ni dalili ya mpasuko mkubwa ndani ya chama unaohusu viongozi wakuu wa chama akiwamo mwenyekiti, makamu mwenyekiti na viongozi wengine wa kitaifa.”
“Tulikuwa tunategemea kwa mfano wangekuwa wamekaa kikao cha dharura kujadili mambo yote hata yaliyotokea kwenye uchaguzi wa Arusha, lakini hatuoni uelekeo wowote, hivyo hisia tunayoipata ni kwamba kuna mpasuko mkubwa kwenye chama,” amesema.
Wakati chama hicho kikiendelea na uchaguzi wa ndani, kumekuwa na hisia kwa baadhi ya viongozi kupanga safu tangu ngazi za chini kuelekea uchaguzi mkuu utakaochagua mwenyekiti wa chama.
Dk Mbunda amesema uchaguzi huo pia ni chanzo cha fukuto hilo.
“Mambo yote kwa sababu ya huo uchaguzi mkuu watu wanapangana ndani kwa ndani, kuna watu walishasema wanataka kugombea vyeo fulani, ndio maana hayo maneno yote yanatoka,” amesema.
Ameonya endapo Chadema isipojipanga vizuri, huenda ikaingia kwenye uchaguzi mkuu wa 2025 ikiwa kwenye mpasuko mkubwa.
Akitoa maoni kupitia mtandao wa X (zamani Twitter), mchangiaji anayejulikana kwa jina la Magiri aliandika… “mambo serious kama uchaguzi lazima kauli itoke juu kabisa, kumsusia chama John Mrema inakatisha tamaa wanachama na wapenda mabadiliko. Chadema badilikeni.”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe amesema ukimya wa Mbowe wakati huu mgumu umeashiria mambo mawili.
“Kwanza, unaonesha hakuna kikao kimekaa kama taasisi kuamua nini kisemwe na nini kisisemwe kwa umma, pili inaonekana kuna mgawanyiko wa viongozi ndani ya chama, yawezekana ukimya wa mwenyekiti yuko chimboni anatafuta suluhisho.
“Ila yote kwa yote haya yalotokea yanaashiria chama kushindwa kufanya kazi kama taasisi,” amesema Dk Kabobe.
Amesema chama hicho kinaonekana kuweka kando utaasisi na kuanza kufanya kazi kama mtu mmoja mmoja.
“Haiwezekani kila mmoja ni msemaji wa chama, kila mmoja anatuhumu mwenzake kila mmoja anatoa kauli ya chama. Kuna mkwamo ndani ya chama wa kutoelewana.
“Wakati huu ni wakati wa kufanya kazi kama taasisi hasa wanapoelekea kwenye chaguzi muhimu za Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani,” amesema.
Mchambuzi wa masuala ya kijamii, Rosemary Mwakitwange amesema kwa jumla chama hicho kimewaangusha Watanzania katika kupigania masuala muhimu ya nchi hususani mabadiliko ya Katiba.
“Tusiangalie tu mwenyekiti, bali nafasi nzima ya upinzani nchini, kwamba umetuangusha,” amesema Mwakitwange.
Amesema wakati ambao Katiba ya Jamhuri ya Muungano ikiweka ushiriki wa siasa kupitia vyama vya siasa, hali hiyo imegawanyika fursa watu wasio wanachama au wapenzi wa vyama.
“Tulidhani kwamba mwakilishi wetu ni vyama vya siasa na ndivyo vingebeba mahitaji yetu, lakini vimeshindwa kubeba matakwa ya wananchi.
“Kwa mfano Chadema, kwa kila jambo linapotokea, wanasema kamati kuu itaamua, hata mambo ya chama chao wenyewe.
“Kama kamati kuu ndio suluhisho la kila kitu, ina maana haiwakilishi matakwa ya wanachama ndio maana wanalalamika, lakini pia tunaoa hata baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wanalalamika, ina maana hata wao hawawakilishwi kwenye mambo yao,” amesema.