Mkutano huo wa siku mbili unaofanyika kwenye mji wa mwambao wa Brazil wa Rio de Janeiro unawaleta pamoja viongozi wa mataifa 20 yaliyostawi zaidi kiviwanda na yale yanayoinukia katika nguvu za kiuchumi.
Jumba la makumbusho ya sanaa mamboleo kwenye fuo za bahari ya Atlantiki mjini Rio ndiyo eneo ambako viongozi wenye usemi duniani wanakutana kujadili ajenda chungunzima za kimataifa kwenye mkutano wao wa kilele wa kila mwaka.
Rais Joe Biden wa Marekani anahudhuria mkutano huo ambao utakuwa wa mwisho kwa sababu atawachia madaraka mnamo mapema mwaka unaokuja.
Viongozi wengine wanaoshiriki mkutano huo ni pamoja na Rais Xi Jinping wa China, Emmanuel Macron wa Ufaransa, Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika na mawaziri wakuu wa Uingereza, Japan na Italia. Kiongozi wa Urusi Vladimir Putin hatohudhuria mkutano huo.
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ambaye nchi yake si mwanachama wa kundi la G20 ni miongoni mwa viongozi walioalikwa kushiriki mkutano huo.
Rais Lula kutoa kipaumbele mapmbano dhidi ya umasikini na njaa duniani
Mwenyeji wa mkutano huo Rais Luiz Inácio Lula da Silva wa Brazil analenga kuutumia kuzindua kile kinatajwa kuwa “Muungano wa Ulimwengu dhidi ya Njaa na Umasikini”.
Kiongozi hiyo anataka kupigia upatu kutolewe ahadi za kifedha kutoka nchi za G20 kusaidia miradi ya uzalishaji chakula na kukabiliana na njaa kila kona ya dunia.
Lula, mwanasiasa msoshalisti, alikiambia kituo kimoja cha televisheni jana Jumapili kwamba angependa kuona mkutano wa Rio unatoa kipaumbele katika kujadili masuala yanayowahusu watu masikini na wale wasio na sauti kote duniani.
Amesema waziwazi kwamba angetamani vita vinavyoendelea duniani hasa vile vya Ukraine na Mashariki ya Kati visiwe sehemu ya ajenda ya mkutano wa G20.
Hata hivyo shauku hiyo ya Lula pengine itaambulia patupu kwa sababu tayari viongozi wengine waliowasili mjini Rio inaonesha wangependa kuutumia mkutano huo kujadili mizozo inayoendelea.
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer ameahidi kwamba suala la Ukraine litakuwa ajenda yake ya juu kwenye mkutano huo na amewaambia waandishi habari kwamba itafaa mataifa washirika yaisaidie Ukraine hadi dakika ya mwisho kwenye vita vyake dhidi ya Urusi.
Mtizamo kama huo umetolewa pia na viongozi wa Ujerumani na Ufaransa na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Bibi Ursula von der Leyen.
Mkutano wa Rio chini ya kiwingu cha mkutano wa mazingira wa COP29
Mkutano wa G20 unafanyika sambamba na mkutano mwingine wa kilele wa mabadiliko ya tabianchi wa COP29 unaoendelea huko Baku, Azerbaijan na mazungumzo yake yamekwama katika suala la kupatikana fedha za kuyasaidia mataifa masikini kukabiliana na athari za kuongezeka joto duniani.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameyatolea mwito mataifa ya G20, ambayo kwa jumla yanabeba asilimia 80 ya utoaji wa gesi chafuzi duniani, kuonesha njia ili kufikiwe makubaliano kwenye mkutano wa COP29.
Chanzo kimoja cha kidiplomasia nchini Brazil kimesema mataifa yanayoendelea kwa kasi kama China, yanakataa miito kutoka mataifa tajiri ya kujiunga katika kuchangia fedha za kupambana na madiliko ya tabianchi. Amesema hata hivyo anatumai mkutano wa Rio unaweza kufungua njia ya masikilizano.
Lakini mashaka bado ni makubwa ikizingatiwa kwamba Donald Trump atarejea madarkani kuiongoza Marekani mwaka ujao na sera zake zinafahamika kwa kuyaweka maslahi ya nchi yake kwanza na kuyapa kisogo masuala ya kimataifa ikiwa ni pamoja na mikataba kama ya mazingira.