Mtoto anusurika kifo akidaiwa kunyweshwa sumu

Musoma. Mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka mitano amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, akidaiwa kunyweshwa sumu ya kukuzia nyanya na jirani yao huku chanzo cha tukio hilo kikiwa bado hakijulikani.

Mtoto huyo aliyefahamika kwa jina la Daniel Edward mkazi wa Mtaa wa Kwangwa A, katika Manispaa ya Musoma, anadaiwa kufanyiwa kitendo hicho Novemba 13, 2024 jioni akiwa nyumbani anakoishi na bibi yake.

Akizungumza na Mwananchi hospitalini hapo leo Jumatatu Novemba 18, 2024, mama wa mtoto huyo, Maryciana Patrice amesema alimkuta mwanaye amelala chini pembezoni mwa nyumba yao, akiwa anatapika matapishi meupe yenye harufu kali.

“Mimi huwa siishi hapa, ila mwanangu anakaa hapa na bibi yake, siku ya tukio nikitokea senta nilimkuta mwanangu akiwa  amelala pembeni ya nyumba huku akitapika matapishi yaliyokuwa yanatoa harufu kali.”

Amesema alimbeba na kumuingiza ndani huku akiwa hajui chanzo na aliendelea kutapika usiku kucha hadi akaishiwa nguvu na kupoteza fahamu.

“Muda wote alikuwa analia tumbo linamuuma alfajiri tukampeleka hospitali ambapo aliwekwa kwenye chumba cha uangalizi maalumu hadi mchana alipozinduka,” amesimulia mama huyo.

Amesema baada ya kuzinduka akiwa bado hana nguvu, walimuuliza alikula nini jana yake, ndipo alipowaeleza kuwa alikunywa maziwa yaliyokuwa kwenye kopo aliyopewa na bibi huyo (huku akimtaja jina) ambaye ni jirani yao.

Mtoto huyo amedai kuwa bibi huyo alimwambia ayanywe kisha aingie ndani akalale.

Bibi wa mtoto huyo, Siwema Malima ambaye ndiye anayeishi naye, amedai kuwa hana ugomvi na jirani yake huyo ingawa hawana uhusiano mzuri kwa muda mrefu sasa.

“Huyo bibi alikataa tusiwe tunamuomba kitu chochote, ikabidi na mimi nimzuie mjukuu wangu asiwe anakwenda nyumbani kwake kucheza na wajukuu zake ingawa sisi ni majirani, yeye ndiye aliamua tusiwe na huo ujirani,” amedai Malima.

Bibi huyo amesema ameanza kuhofia usalama wa mjukuu wake huyo hasa ikizingatiwa kuwa nyumbani kwake wanaishi watatu tu yeye na mjukuu wake na mtoto wake wa mwisho anayesoma darasa la tano, huku mama wa mtoto huyo akiishi kijijini na mume wake.

Amesema wakati akiendelea kumuuguza mjukuu wake hospitalini pia amelazimika kuhamishia familia yake kwa ndugu.

Hata hivyo, amesema tayari walishatoa taarifa Polisi katika Kituo cha Musoma na mtuhumiwa alikamatwa, lakini kwa sasa yuko nje kwa dhamana.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara,  Nernard Sindano amesema hana taarifa za tukio hilo huku akiahidi kufuatilia ili kujua undani wake.

Daktari wa wodi ya watoto hospitalini hapo, Majaliwa Ayubu amesema hali ya mtoto huyo hivi sasa inaendelea vizuri tofauti na walivyompokea.

“Alikaa kitengo cha dharura kwa zaidi ya saa 10 kabla ya kuhamishiwa wodini, hali yake ilikuwa mbaya sana, kwanza alikuwa amepoteza fahamu na alikuwa dhaifu sana na hata fahamu ilipomrudia alikuwa anapumua kwa taabu huku akitokwa machozi bila kulia.”

“Pia alikuwa anatapika mara kwa mara matapishi yenye harufu kali,” amesema daktari huyo.

Mwananchi lilimtafuta pia mtuhumiwa wa tukio hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Nyamakunja ambaye amekiri kukamatwa na Polisi akihusishwa na tukio hilo, ingawa amekanusha tuhuma hizo.

Pia amedai kutokumfahamu mtoto huyo kwa maelezo kuwa sio kweli kuwa mtoto huyo anaishi na bibi yake jirani na yeye.

Lakini baada ya muda mfupi, bibi huyo alisema anamfahamu mtoto kuwa anaishi eneo la kijijini na mama yake mzazi na Jumapili, mama wa mtoto akiwa ameambatana na mtoto huyo, walienda kumuomba ampatie dawa ya kienyeji akieleza kuwa mtoto wake anaumwa degedege, ombi ambalo bibi huyo alilikataa.

“Nilimuuliza unaniomba dawa kwani mama yako yuko wapi, akasema ameenda kumtafutia dawa nyingine, baada ya kumkatalia akaniomba maembe nikamwambia achume na baadaye  wakaondoka na mtoto wake,” amesimulia na kuongeza;

“Siku ya tukio ambayo wanasema nilimpa sumu huyo mtoto, mimi sikushinda  hapa nyumbani, sasa huyo mtoto mimi nilimnywesha hiyo sumu saa ngapi, nani aliniona? alete na ushahidi,” amesema bibi huyo.

Related Posts