Dar es Salaam. Serikali imesema bado inaendelea na uchunguzi katika kesi ya wizi wa shehena ya mafuta ya petrol na dizel yenye uzito wa jumla ya lita 9.9 milioni, inayomkabili dereva wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Tino Ndekela na wenzake saba.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka 20 akiwemo ya kutakatisha fedha na wizi wa mafuta ya petrol na dizel zaidi ya lita 9.9milioni na kuisababishia hasara Kampuni ya Kimataifa ya kuhifadhi Mafuta (Tiper) ya zaidi ya Sh26 bilioni.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi ni mfanyabiashara Fikiri Kidevu, Amani Yamba, Mselem Abdallah , Kika Sanguti, Twaha Salum, Gaudence Shayo na Hamisi Hamisi.
Leo, Jumatatu Novemba 18, 2024, Wakili wa Serikali, Titus Aaron ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea hivyo wanaomba tarehe nyingi kwa ajili ya kutajwa.
Wakili Aaron ametoa maelezo hayo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki, anayesikiliza shauri hilo.
Kutokana na upelelezi kutokamilika, mahakama imepanga Desemba 2, 2024 kesi hiyo itaitwa kwa ajili ya kutajwa.
Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shitaka la kutakatisha fedha linalowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.
Katika mashitaka hayo, mawili ni ya uharibifu wa mali wanaodaiwa kutenda kati ya Januari Mosi, 2019 na Desemba 31, 2022 eneo la Tungi, Kigamboni ambapo waliharibu bomba la kusafirishia mafuta aina ya petroli na dizeli mali ya Kampuni ya Tiper.
Pia washtakiwa hao, wanakabiliwa na mashitaka 16 ya wizi wa mafuta ambapo wanadaiwa kuiba lita 3,599,458 za mafuta ya aina ya petroli na lita 6,392,356 za mafuta ya dizeli yaliyokuwa yakishushwa kutoka katika meli na kuingizwa katika visima vya kampuni hiyo.
Vilevile, wanakabiliwa shitaka la kuisababishia hasara kampuni hiyo ya Sh26.01 bilioni. tukio wanalodaiwa kulitenda katika kipindi hicho eneo la Tungi, Kigamboni, Dar es Salaam.
Washtakiwa hao, pia wanakabiliwa na shitaka moja la kutakatisha Sh20.73 bilioni, tukio wanalodaiwa kulitenda katika tarehe hizo na eneo hilo, huku wakijua fedha hizo zilitokana na kosa tangulizi la wizi.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Oktoba 22, 2024 na kusomewa mashitaka yanayomkabili.