Serikali kutatua changamoto ya mashine ya kuchakata mkonge Tanga

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Suleiman Serera amekutana na viongozi wa Vyama vya Ushirika na Masoko vya Mkonge (AMCOS) katika wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, ambapo ameahidi kutatua changamoto zinazoikumba sekta ya mkonge, hususan uhaba wa mashine zinazotumika kuchakata zao hilo maarufu kama makorona.

Katika kikao hicho, kilicholenga kujadili mbinu za kuboresha uzalishaji na usindikaji wa mkonge, Serera amesisitiza kuwa “serikali iko makini katika kuhakikisha wakulima wa mkonge wanapata vifaa vya kisasa vitakavyorahisisha kazi zao na kuongeza thamani ya mazao yenu
wizara hii ipo tayari na imeanza kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na taasisi za kifedha na mashirika ya maendeleo na tayari Serikali imetenga fedha kwaajili ya kuufanikisha upatikanaji wa mashine hizo na kuimarisha uchumi wa wakulima”

Kwa upande wao, viongozi wa AMCOS walimshukuru Naibu Katibu Mkuu kwa hatua hiyo na kuomba juhudi hizo zifanyike kwa haraka ili kutatua changamoto za muda mrefu zinazowakabili ikiwepo changamoto ya barabara za kupita kwenye mashamba yao kutokana na ukubwa wa mashamba hayo.

Pia Serera pia ametoa wito kwa wakulima kuendelea kushirikiana na vyama vya ushirika kwa karibu, akisema kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kufanikisha maendeleo ya kilimo na ustawi wa wakulima wote.

Related Posts