Serikali mbioni kuwasomesha watoto familia zinazonufaika na Tasaf

Katavi. Serikali ipo kwenye mpango mkakati wa kusaidia wanafunzi kutoka familia wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini.

Lengo ni kuhakikisha wanaendelea  na masomo ya elimu ya juu na mafunzo ya ufundi katika vyuo vya ufundi (Veta) vilivyopo hapa nchini.

Akizungumza leo Novemba 18, 2024 baada ya kutembelea mradi wa barabara yenye urefu wa kilomita 0.5 uliotekelezwa na wanufaika wa Tasaf katika kata ya Ilembo Manispaa ya Mpanda Mkoani katavi, Naibu waziri ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,  Deusi Sangu amedokeza kuhusu mpango huo.

Amesema kumekuwa na changamoto kadhaa ambazo zinawakabili watoto wanaotoka kwenye familia masikini kwa kushindwa kuendelea na masomo,  hivyo kwa kutambua hilo Serikali imejipanga kuanza kuendeleza wanafunzi hao, kupitia ofisi ya Waziri Mkuu ili waweze kujiunga na vyuo vya ufundi pamoja na kupata mikopo ya elimu ya juu.

‘’Tangu mpango wa kusaidia kaya masikini ulipoanza kumekuwa na mafanikio makubwa kwa wanufaika kuinuka kiuchumi na kuanza kufanya biashara ndogondogo zinazowaingizia kipato, pamoja na idadi ya watoto kuandikishwa shule imeongezeka tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma wakati mpango huu unaanza,” amesema.

“Kwa sasa watoto kutoka familia zinazonufaika na mradi wa Tasaf wanamaliza elimu ya msingi na sekondari, lakini wanashindwa kuendelea na elimu ya juu kutokana na kukosa fedha, hivyo Serikali imekuja na mkakati wa kuwaendeleza wanafunzi kutoka familia zinazonufaika ili waweze kuendelea na elimu ya juu.”

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya Tasaf Mtendaji wa Kata ya ilembo amesema kata hiyo imetekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya barabara ambayo imejengwa na wanufaika, huku changamoto kubwa ikiwa ni kuwepo kwa idadi kuwa ya wahitaji wa kuingizwa kwenye mpango tofauti na kipindi cha nyuma.

“Tunaomba Serikali iangalie namna ya kuanza upya uandikishaji wa wahitaji, kwani idadi ya familia ambazo hazijaandikishwa kwenye awamu ya tatu ya mpango wa Tasaf ni nyingi jambo ambalo limekuwa likileta malalamiko mengi kwa wananchi kuwa wametengwa na Serikali kwa kuwa wanastahili kupata fedha hizo,” amesema Jackline.

Related Posts