Dar es Salaam. Serikali imesema kwa sasa inaimarisha miundombinu ya umeme jijini hapa hatua inayosababisha kukosekana kwa huduma ya nishati hiyo katika baadhi ya maeneo jijini hapa.
Kauli ya Serikali inakuja baada ya uwepo wa taarifa na malalamiko ya kukosekana kwa huduma hiyo mara kwa mata katika baadhi ya maeneo yakiwamo Mkuranga, Dege Kigamboni, Mbagala na Gongo la Mboto.
Hayo yamebainishwa leo, Novemba 18, 2024 na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga alipotembelea kituo cha kuzalisha umeme unaotokana na gesi asilia cha Kinyerezi One, kuangalia utekelezaji wa miradi ya kuboresha upatikanaji wa umeme jijini Dar es Salaam.
“Matumizi ya umeme yamekuwa yakipanda kwa kasi kubwa ndio maana tumekuwa na miradi ya kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme Dar es Salaam kila baada ya muda, wengi mtajiuliza kwa nini umeme umekuwa ukizimwa siku tatu zilizopita hususan maeneo ya Mkuranga, Dege Kigamboni, Mbagala na Gongo la Mboto.”
Kuhusu utatuzi wa changamoto hiyo Kapinga amesema, “kuna miradi tunaitekeleza ili kuboresha upatikanaji kuanzia hapa Kinyerezi kwa kuweka transfoma mbili zenye ukubwa ya MVA 175 kwa ajili ya kuongeza ukubwa wa kituo. Kuna njia ya kusafirisha umeme kutoka Kinyerezi kwenda Gongo la Mboto Megawati 150 kutoka Megawati 50”
Amesema pia upo mradi wa kuboresha vituo vya kupooza umeme vya Mbagala na Gongo la Mboto ambapo wataongeza transfoma yenye ukubwa wa MVA 120.
“Tunafahamu wananchi wa maeneo hayo wamekuwa wakilalamika wanashindwa kupiga pasi na shughuli nyingine kwa sababu ya umeme mdogo. Tunaboresha maeneo hayo yote,” amesema.
Kapinga amesema umeme upo wa kutosha changamoto iliyopo baadhi ya maeneo umeme haujitoshelezi kutokana na mahitaji kuongezeka.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga amesema jiji la Dar es Salaam linalisha mikoa ya Pwani na Visiwa vya Zanzibar hivyo mahitaji ya umeme ni makubwa.
Amesema matumizi ya umeme yamekuwa makubwa kutokana na viwanda vingi kuongezeka maeneo ya Mkuranga, hivyo baada ya kukua kwa mahitaji miundombinu inazidiwa.
“Kwa wastani mahitaji ya matumizi ya umeme kwa miaka iliyopita ilikuwa asilimia sita, ila kuanzia mwaka jana hadi mwaka huu imefikia asilimia 16,”amesema.
Amefafanua kuwa siku tatu zilizopita walipotangaza marekebisho walikuwa wanatengeneza miundombinu.
“Kwa siku hizi tatu tulipunguza ugawaji wa umeme katika jiji la Dar es salaam kwa sababu tulikuwa tukifungua mitambo katika kituo cha Kinyerezi, kuirekebisha na kuiandaa ili kuunganisha na transfoma hizo kubwa mbili,” amebainisha.