Dar es Salaam. Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua nzuri aliyoichukua ya kutuma wajumbe wake na kurejeshwa kwa huduma za kijamii kwa wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro.
Pamoja na hayo wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kutimiza ahadi yake ya kutembelea Tarafa ya Ngorongoro, ili kuwasikiliza wananchi na kupata uelewa kamili wa changamoto wanazokabiliana nazo.
THRDC wametoa rai hiyo kutokana na hali ya haki za binadamu katika tarafa hiyo, wakisema uamuzi huo wa kutuma watu wa kusikiliza vilio vya wananchi na kuagiza vifanyiwe kazi umeonyesha busara na hekima ya Rais.
Hayo yameelezwa kwenye tamko hilo lililotolewa leo Jumatatu, Novemba 18, 2024 na Mratibu Taifa, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, Wakili Onesmo Olengurumwa.
Hata hivyo, akizungumza jana Jumapili, Novemba 17, 2024 wakati akitoa tathmini ya utendaji wake wa miezi sita, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda alisema Rais Samia Jumapili ya Desemba Mosi, 2024 anatarajiwa kuwa jijini Arusha, kuzungumza na viongozi wa jamii ya kimasai wanaoishi Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha.
Makonda alisema lengo la ziara hiyo ni kuwasikiliza na kujadiliana kwa pamoja kuhusu changamoto za jamii hiyo, ndani ya Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro.
Olengurumwa amesema kwa muda mrefu watetezi wa haki za binadamu wamekuwa wakishauri uongozi wa juu wa nchi ukutane na wananchi na mara baada ya Rais kutuma wajumbe wake, wameanza kuona faida ya hatua hiyo.
Katika taarifa yake awali amesema huduma mbalimbali za jamii kama vile za mabweni kwa shule za msingi na sekondari, huduma za vyoo mashuleni, afya, barabara, huduma za maji, vibali vya ujenzi na huduma nyinginezo zilififishwa.
“Pamoja na kwamba Serikali ndio imelalamikiwa kusababisha changamoto hizi, kitendo cha Rais kuamua vikwazo hivi viondolewe imeleta matumaini mapya kwa watu wa Ngorongoro, kimetufurahisha sisi watetezi wa haki za binadamu na pia hatua hii inalinda taswira ya nchi katika eneo la haki za binadamu na utawala bora,” amesema.
Amesema baada ya kufanya ziara Novemba mwaka huu, THRDC imejionea hali ya haki za binadamu pamoja na huduma za kijamii katika tarafa ya Ngorongoro.
“Tunatambua na kuthamini juhudi za hivi karibuni zilizofanywa na Serikali kurejesha huduma muhimu za kijamii katika Tarafa ya Ngorongoro, eneo ambalo liliathiriwa kwa kiasi kikubwa na kusitishwa kwa huduma hizi kwa takriban mwaka mzima.
“Kusitishwa kwa huduma hizo hasa kuanzia mwaka 2022 kuliathiri jamii za asili na wafugaji katika eneo hilo ambalo ni mseto,” amesema.
Pamoja na kwamba bado ukarabati wa maeneo mengi ya huduma za kijamii haujaanza, THRDC wameshuhudia mikakati na hatua za awali za urejeshwaji wa huduma za msingi kama huduma za afya, elimu na miundombinu ya msingi.
Olengurumwa ametaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na Halmashauri iliunda kamati maalumu ya kwenda kuzunguka katika Tarafa ya Ngorongoro kwa lengo la kutambua mahitaji ya awali ya haraka katika kufanyia kazi maagizo ya Rais, kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi hao.
Pia amesema wametengewa bajeti na katika eneo la demokrasia na uchaguzi wapiga kura waliosajiliwa, Tarafa ya Ngorongoro inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na idadi kubwa ya wapiga kura waliosajiliwa kwa uchaguzi wa 2024/2025.
“Hii inaonyesha kuwa kuna wananchi wa Tanzania katika eneo hilo na ni vyema kwao kutumia haki yao ya kidemokrasia. Pamoja na hayo, wana Ngorongoro sasa wanahisi kuwa na uhuru wao na uwepo wa viongozi wao wa Serikali baada ya muda mrefu.”
“Pia huduma za elimu imefanywa kwa hatua kidogo, ila bado mengi yanatakiwa kufanyika. Kwa sasa, kuna mifuko ya simenti tayari imewekwa kwenye baadhi ya shule, tayari kwa kuanza ujenzi,” amesema.
Wito kukutana na wananchi
Olengurumwa amesema kukutana na wananchi hao kutatoa nafasi nzuri ya kujadili namna bora ya kuendesha mikakati yote ya kulinda hifadhi kwa kushirikisha wananchi, pia kwa kuzingatia haki za binadamu na utawala bora.
Pia ameshauri shughuli ya kuhamisha watu katika eneo hilo lisitishwe ili kutoa nafasi ya kujipanga upya kwa kutoa nafasi kubwa ya wananchi kushirikishwa na kufanyia kazi mapendekezo ya wadau mbalimbali, wakiwemo watetezi wa haki za binadamu.
“Tunashauri kuacha kutoa vitisho kwa watetezi na waandishi wa habari wanaofuatilia haki za wananchi katika eneo hili. Badala yake wapewe ushirikiano na mamlaka zote zinazohusika na eneo hili.
“Serikali na mamlaka zote ziendelee kuheshimu na kulinda haki za wananchi ambao hawajaamua kuhama kwa kwenda maeneo mengine. Pia jitihada za kuboresha huduma za jamii zifanyike kwa haraka, mfano shule zote zifanyiwe ukarabati wakati huu ambapo wanafunzi wanafunga shule,” amesema.
Pamoja na hayo amesema bajeti iliyotengwa inaonyesha ni ya kufanya ukarabati pekee, hivyo wanashauri Tarafa ya Ngorongoro itengewe fedha kubwa toka serikalini na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), ili kuboresha na kuongeza miundombinu mingine ambayo kwa sasa inakosekana katika huduma zote za kijamii.