Vifo ghorofa lililoporomoka Kariakoo vyafikia 16

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema bado kuna sauti za watu wanawasiliana nao ndani ya jengo la ghorofa lililoporomoka kwenye soko Kuu la Kariakoo, huku akithibitisha kutokea vifo 16 na majeruhi 86 hadi sasa.

Hata hivyo, leo katika tukio la kuaga miili ya waathirika wa ajali hiyo iliyofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi mmoja,  miili 15 ndiyo imeagwa, ambapo Majaliwa  ameeleza kuwa mwili mmoja ulichukuliwa na ndugu kabla ya tukio la kuaga.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Majali amesema hadi leo Novemba 18, 2024 watu 86 walikuwa wameokolewa.

“Majeruhi wote walipatiwa matibabu kwenye Hospitali za Muhimbili, Baracks Kilwa Road, Amana, Aga Khan na Mnazi Mmoja na wengi wao wanaendelea vizuri.” “Ndugu zetu 16 walipoteza maisha, hapa kuna miili 15, mmoja ulishachukuliwa,” amesema.

Waziri Mkuu amesisitiza, Serikali itaendelea kuchukua hatua kunusuru maisha ya watu waliomo ndani ya jengo hilo na shughuli ya uokoaji inaendelea.

Amesema hatua ya uokozi hadi sasa ipo chini ya shimo la jengo hilo la ghorofa tatu na eneo la chini la ghorofa moja lililoporomoka Novemba 16, 2024 saa 3 asubuhi.

“Bado tunapata sauti za Watanzania walioko huko chini, hadi leo saa 5 asubuhi (Novemba 18) walikuwa wanawasiliana nasi,” amesema Majaliwa.

Amesema wanaendelea na uokozi na watu hao wamepelekewa hewa safi, maji na glucose wakati shughuli ya  kuwaokoa ikiendelea.

“Shughuli ya uokozi ifanyike  

usiku na mchana isisimame hadi kuhakikisha mtu wa mwisho ndani ya jengo hilo anaokolewa.”

“Tuombe Mungu wenzetu hawa watoke salama, ambacho Serikali inaendelea kukifanya ni kugharamia matibabu kwa majeruhi na waliopoteza maisha, imetoa majeneza, sanda na gharama za maziko kwa marehemu wote,” amesema.

Waziri Mkuu pia ameagiza viongozi wa Serikali kwenye maeneo yote ambayo miili hiyo itakwenda kuzikwa kushiriki kikamilifu kwenye mazishi hayo.

“Sambamba na hilo, tunakamilisha taratibu za uchunguzi maalumu wa chanzo cha ajali hii, nimeagiza Jeshi la Polisi kumtafuta mwenye jengo, ili kuisaidia kuwapa polisi majibu ya kwa nini jengo limeanguka na yeye atajibu swali moja baada ya jingine,” amesema.

Aidha ameunda timu ya watu 19 ambao watayapitia maghorofa yote  ya Kariakoo kujua ubora na shughuli zinazoendelea kwenye soko hilo.

“Timu hii itasaidia kujua na kuishauri Serikali nini ifanye, tunafahamu mahitaji ya Soko la Kariakoo yapo palepale, tunayo sababu ya kuimarisha na kutambua ubora wa majengo tuliyonayo,” amesema akimtaja Mwenyekiti wa timu hiyo kuwa ni Brigedia Jenerali, Hosea Ndagara na katibu wake ni, Mhandisi Meleck Mwano.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameliagiza Jeshi la Polisi kumtafuta na kumkamata mtu aliyemtaja kwa jina la Jennifer Jovin ili aseme ametumwa na nani kuchangisha michango ya maafa ajali ya ghorofa lililoporomoka Kariakoo.

Amesema, mtu huyu atafutwe aseme nani amempa kibali cha kukusanya michango hiyo na amekusanya kiasi gani?

“Shughuli yoyote ya maafa ina utaratibu, huyu mtu kama anasikia bora atangulie mwenyewe Polisi,” amesema Waziri Mkuu kwa msisitizo akiwa katika tukio la kuaga miili ya watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo.

“Wale wanaotumia fursa ya ajali hii kuwachangisha Watanzania waache mara moja, shughuli yoyote ya maafa ina utaratibu,” amesema Majaliwa.

Akitoa taarifa ya ajali na uokozi, Mwenyekiti wa kamati ya maafa, William Lukuvi amesema ajali hiyo imesababisha madhara ya binadamu, mali na miundombinu.

Amesema uokozi wa watu waliokwama chini ya kifusi unaendelea na uchunguzi kubaini chanzo ha jengo hilo kuporomoka unaendelea.

Related Posts