Waliofariki ajali ya Kariakoo waagwa – DW – 18.11.2024

Miili ya wahanga 15 wa tukio hilo ilifikishwa kwenye viwanja hivyo ikiwa imebebwa na wanajeshi wa Jeshi la Wananchi kwa ajili ya kuagwa kabla ya kuzikwa, kufuatia kisa hicho kilichotokea Novemba 16, 2024.

soma zaidi:Jengo laporomoka na kuuwa kadhaa Kariakoo Dar es Salaam

Waziri Mkuu wa nchini Tanzania Kassim Majaliwa ameongoza shughuli ya kuaga miili hiyo, iliyohudhuriwa na waombolezaji waliojitokea zwa wingi, na waliogubikwa na huzuni kubwa.

Juhudi za uokozi zimeendelea ili kuwaokoa waliokwama kwenye kifusi cha jengo hilo wakati ndugu, jamaa na marafiki wakiendelea kupokea  jumbe mbalimbali za wenzao walionaswa kwenye kifusi wakiomba msaada na baadhi wakiwaaga wakiashiria kuwa pengine hawataonana tena.

Samia Suluhu Hassan | Rais wa Tanzania
Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza kufanyika tathmini ya majengo yaliyoko Kariakoo jijini Dar es Salaam baada ya kisa cha kuporomoka za jengoPicha: Daniel Pier/NurPhoto/picture alliance

Rais Samia Suluhu Hassan aagiza uchunguzi zaidi wa majengo

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ameagiza timu ya uokoaji iongezwe katika eneo hilo la Kariakoo ili kuharakisha zoezi hilo na kufanikisha kuwaokoa.

Idadi ya waliokwama haikuwa wazi, lakini baadhi ya watu wameviambia vyombo kadhaa vya habari nchini humo kwamba wamepoteza mawasiliano na jamaa zao ambao wanaamini bado wako chini ya jengo hilo lililoanguka.

Zaidi ya watu 80 wamekwishaokolewa kutoka chini ya jengo hilo la ghorofa nne lenye maduka. Kulingana na Rais Suluhu siku ya Jumapili, watu 26 walikuwa wanapatiwa matibabu hospitalini na serikali ikaahidi kulipia gharama za tiba na mazishi.

Kiongozi huyo aidha aliagiza majengo yote yaliyoko kwenye eneo la Kariakoo kufanyiwa tathmini. Eneo hilo linasifika kwa biashara mbalimbali.

Majengo hushuhudiwa kuanguka katika nyakati za mvua, lakini pia kumekuwepo na matukio kama hayo katika baadhi ya miji ya Afrika kwa sababu ya viwango duni vya ujenzi.

Soma pia:Serikali ya Tanzania yaunda tume na wafanyabiashara

Related Posts