WAZIRI wa Madini, Mheshimiwa, Anthony Mavunde amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuendelea kusimamia sheria kwenye utendaji kazi ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza kati ya wachimbaji wa madini na ajali kwenye shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini.
Waziri Mavunde ametoa rai hiyo kwenye kikao kazi cha menejimenti ya Tume ya Madini kilichofanyika mapema leo Novemba 18, 2024 chenye lengo la kuweka mikakati ya kuendelea kuimarisha Sekta ya Madini kuanzia kwenye ukusanyaji wa maduhuli, usimamizi wa sheria, biashara ya madini na mchango wake kuendelea kukua kwenye Pato la Taifa.
Amesema kuwa kuendelea kusimamia sheria katika utendaji kazi kumewasaidia Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa wengi kuwepo hapa leo hii.
Katika hatua nyingine amepongeza kasi ya ukusanyaji wa maduhuli inayofanywa na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa na kuwataka kuendelea kuwa wabunifu hasa kwenye udhibiti wa mianya ya upotevu wa mapato.
Wakati huohuo Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amewaagiza wakaguzi migodi kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye migodi hususan kipindi hiki cha mvua ili kuepusha majanga migodini.
“Kuanzia kipindi hiki mpaka Aprili mwakani ni kipindi cha mvua, mfanye ukaguzi mara kwa mara, migodi isiyoridhisha ifungiwe hadi itakapoboreshwa, hatutavumilia vifo vya uzembe migodini,”amesema Mhandisi Samamba.
Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kutimiza majukumu yao sio tu kufikia lengo la Shilingi Trilioni moja, malengo yapo mengi na makubwa na kwamba sekta ya madini inatakiwa kuchangia kwenye pato la Taifa kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.
“Tufanye udhibiti wa kutosha, tukasimamie sheria, kanuni na taratibu tutafikia mchango wa asilimia 10 na kuzidi,”amesisitiza Mbibo.
Katika hatua nyingine, Mbibo ameelekeza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuangalia namna bora ya kudhibiti mianya ya utoroshaji wa madini hasa kwenye maeneo ya mipakani na viwanja vya ndege.