161,020 wakacha mtihani kidato cha nne

Mpango wa elimu bila malipo uliobuniwa na Serikali umelenga kupanua fursa za elimu kwa watoto wote nchini.

Hata hivyo, takwimu zinaonyesha kuwa changamoto za kielimu bado ni kubwa, hasa kutokana na tatizo la wanafunzi kuacha shule katikati ya safari ya masomo.

Hii ni changamoto inayoonekana wazi, hasa kwa vijana walio na umri wa kwenda shule ambao badala ya kuwa darasani wanajishughulisha na kilimo, ufugaji, au biashara ndogo kama kuendesha bodaboda.

Hali hii, inayojulikana kitaalamu kama “mdondoko,” inadhihirisha changamoto kubwa kwa jamii na maendeleo ya Taifa.

Akizungumza kuelekea kuanza kwa mtihani wa Taifa wa kidato cha nne wa mwaka 2024, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), Dk Said Mohamed, alitoa takwimu za kutisha

Alibainisha kuwa jumla ya wanafunzi 161,020, sawa na asilimia 23.3 ya waliotarajiwa kufanya mtihani huo, hawakuandikishwa.

 Wanafunzi hawa, ambao walifanya mtihani wa kidato cha pili mwaka 2022 wakiwa 690,341, walipungua hadi 529,321 walioandikishwa kwa mtihani wa kidato cha nne mwaka huu.

“Kuna upungufu wa wanafunzi ambao walitakiwa kuandikishwa kufanya mtihani huu lakini hawapo katika orodha ya waliosajiliwa mwaka huu,” alisema Dk Mohamed.

Kwa mujibu wa ripoti ya Takwimu za Elimu Msingi Tanzania (BEST) ya mwaka 2024, idadi ya wanafunzi wa shule za msingi wanaoacha shule imepungua kwa asilimia 18.19 kati ya mwaka 2022 na 2023. Idadi hiyo ilishuka kutoka 193,605 mwaka 2022 hadi 158,372 mwaka 2023.

 Kwa upande wa sekondari, idadi ya wanafunzi waliokatisha masomo iliongezeka kwa asilimia 10.01 kutoka 134,295 mwaka 2022 hadi 147,741 mwaka 2023.

Hii inaashiria kuwa, ingawa hatua za Serikali zimeleta matokeo mazuri katika kupunguza mdondoko wa wanafunzi wa shule za msingi, changamoto hiyo imezidi kuonekana kwa wanafunzi wa sekondari.

Ripoti hiyo pia ilifafanua kuwa wanafunzi wa darasa la nne, kidato cha kwanza na kidato cha pili, walichangia asilimia 55.6 ya wanafunzi wote walioachaa shule mwaka 2023.

 Hii ni ishara ya changamoto kubwa katika madarasa haya ambayo inahitaji kushughulikiwa kwa kina.

Mtaalamu wa masuala ya elimu na mchambuzi, Dk Roze Matete kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, anaeleza kuwa hamu ya kusoma kwa watoto wengi imepungua kutokana na mzigo wa majukumu wanaopewa nyumbani na wazazi wao, ambao mara nyingi wanawatuma kufanya kazi za nyumbani badala ya kuwa shuleni.

“Ni kawaida sana mtoto kurudi nyumbani na kukutana na majukumu ya familia, hasa kama kuna shughuli za kifedha kama kilimo, biashara au madini,” anasema Dr. Matete.

 Anaongeza kuwa, mzazi ana nafasi kubwa ya kushawishi hamu ya mtoto katika elimu, huku akitolea mfano wa daktari bingwa wa upasuaji nchini Marekani, Dk Ben Carson, aliyefikia mafanikio hayo kwa ushawishi mkubwa wa mama yake.

Mwalimu mzoefu, Richard Mabala, anasema umasikini ni sababu kuu ya mdondoko wa wanafunzi.

“Wanafunzi wengi wanatoka katika familia maskini na wanahisi kuwa msaada wao wa kifedha ni muhimu zaidi kwa familia zao kuliko elimu,” anasema.

Mabala anaeleza kuwa, licha ya mpango wa elimu bila malipo wa Serikali, familia nyingi zinabeba gharama za sare, vitabu, na usafiri wa watoto wao.

“Gharama hizi, ingawa si za moja kwa moja, zinaweza kuwa mzigo mkubwa kwa familia maskini, na hili huwafanya watoto wengine kuacha shule,” anafafanua.

Naye mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Oscar Mkude, anasema changamoto si tu ada za shule, bali pia gharama za usafiri, sare, na vifaa vya kusomea.

“Hapa ndipo Serikali na sekta binafsi zinatakiwa kuongeza nguvu,” anasema Mkude na kushauri kuanzishwa kwa mpango madhubuti wa msaada wa kifedha kwa familia zenye kipato kidogo kupitia programu kama Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (Tasaf).

“Sekta binafsi inaweza kushirikiana na Serikali kuhakikisha kila mwanafunzi ana fursa ya kuendelea na elimu bila kujali changamoto za kifedha za familia yake,” anasisitiza.

Katika nchi zilizoendelea, serikali pamoja na sekta binafsi zimekuwa zikiwasaidia wanafunzi na familia zenye kipato cha chini kwa kutoa vifaa vya kusomea bure, kutoa posho kwa wazazi au walezi, na kuweka usaidizi wa kisaikolojia kwa watoto ili kuhakikisha wanakabiliana na changamoto za masomo kwa ufanisi.

Nchi hizi zina mipango ya kubaini changamoto za watoto mapema, kuhakikisha hawafeli au kukata tamaa, na kuandaa mwongozo wa kitaaluma na kisaikolojia kwa kuwasaidia wanafunzi wenye changamoto maalumu.

Nchi kama Finland, kwa mfano, imefanikiwa kuanzisha mifumo ya msaada wa kijamii inayowezesha kila mtoto kupata elimu bora kwa msaada wa kifedha, kisaikolojia, na kimazingira.

Kwa upande wa Tanzania, kuandaa watoto kuelekea sekondari ni muhimu katika kupunguza mdondoko wa wanafunzi.

Njia mojawapo inayoweza kuzuia mdondoko huu ni lugha ya kufundishia. Ukweli ni kuwa mwanafunzi anayetoka msingi akiwa amefundishwa kwa Kiswahili, anapata wakati mgumu kusoma sekondari anapokumbana na lugha ngeni. Baadhi hutumia kigezo hiki kama sababu ya kukacha masomo.

 Katika juhudi za kukabiliana na changamoto hii, serikali ilianzisha programu ya kuboresha ujuzi wa lugha ya Kiingereza kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza mnamo mwaka 2022, lakini wataalamu wanahimiza kuwepo kwa mipango zaidi ya kuwaandaa wanafunzi kitaaluma na kisaikolojia wanapoingia sekondari.

Mbali na maandalizi ya lugha, shule nyingi nchini hazitoi fursa za kutosha kwa watoto wanaopenda sanaa, michezo, na vipaji vingine nje ya mtaalaa rasmi.

Mdau wa elimu, Moses Kyando, anasema kuwa mfumo wa elimu umekuwa ukithamini sana masomo ya vitabu na kuandika huku ukiacha nje stadi za maisha na vipaji walivyo navyo watoto.

“Wapo watoto wengi wanaopendelea sanaa, michezo, na shughuli za ufundi, lakini shule nyingi hazina mpango wa kukuza vipaji hivyo, jambo linalowakatisha tamaa watoto wasio na uwezo mkubwa wa kitaaluma,” anasema.

Anatoa mfano wa baadhi ya watoto wanaoacha shule na kujikita katika kuimba, ufugaji, na michezo kwa sababu wanajiona hawana nafasi ya kufaulu katika masomo ya darasani.

Uchambuzi wa takwimu za elimu unaonesha kuwa, pamoja na kupungua kidogo kwa mdondoko wa wanafunzi mwaka 2023, bado kuna idadi kubwa ya wanaoacha shule ambayo wanahitaji hatua za haraka kusaidiwa.

Kwa mujibu wa wataalamu wa elimu, juhudi za kuzuia mdondoko huu zinaweza kuimarishwa kwa kuongeza msaada kwa familia maskini, kujenga mfumo wa elimu unaojumuisha michezo na sanaa, na kuwapa wanafunzi msaada wa kisaikolojia.

Pia, wazazi wanapaswa kutambua kuwa elimu ni njia bora ya kuwapa watoto wao maisha bora ya baadaye, na hivyo wanahitaji kuwa na hamasa kubwa ya kuhakikisha watoto wao wanasoma bila kupewa majukumu yanayowakwamisha kufikia malengo yao ya kielimu.

Kwa ujumla, mdondoko wa wanafunzi ni changamoto inayohitaji suluhisho endelevu. Ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, wazazi, jamii, na sekta binafsi unaweza kuleta mabadiliko makubwa kwa watoto hawa, na hivyo kusaidia kufanikisha ndoto za vizazi vijavyo na kuleta maendeleo kwa Taifa.

Kwa upande mwingine, Tanzania inaweza kupunguza tatizo hili kwa kuzingatia hatua zinazochukuliwa na nchi zilizoendelea, na kufanya mabadiliko yenye manufaa katika mfumo wa elimu.

Related Posts