Dar es Salaam. Wakati kesho Jumatano, Novemba 20, 2024 kampeni za uchaguzi wa Serikali za mitaa zinaanza, Chama cha ACT Wazalendo kimeweka hadharani safu yake ya viongozi watakaofanya kampeni nchi nzima.
Kampeni hizo zitakazohitimishwa Novemba 26, 2024, mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Juma Duni Haji amekabidhiwa Mkoa wa Dar es Salaam na atafanya mikutano 28. Uchaguzi wenyewe ni Jumatano ya Novemba 27, 2024.
Msemaji wa uchaguzi wa Serikali za mitaa wa chama hicho, Rahma Mwita akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho, Magomeni jijini Dar es Salaam kuhusu uchaguzi huo, amesema viongozi wa kitaifa wakiongozwa na kiongozi wa chama, Dorothy Semu wanatarajiwa kushiriki kwenye kampeni hizo.
Rahma amesema kiongozi wa chama, Dorothy Semu na Makamu Mwenyekiti Bara, Isihaka Mchinjita wataongoza kampeni katika mikoa ya mkoa wa kichama Mwambao, Lindi, Mtwara na Selous.
Amesema kiongozi mstaafu, Zitto Kabwe na Mwenyekiti Ngome ya Wanawake, Janeth Rithe na Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana, Abdul Nondo, wataongoza kampeni katika mikoa ya Tabora, Katavi, Rukwa na Tabora.
Amesema Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Ismail Jussa na mjumbe wa kamati Kuu, Rehema Ally wataongoza kampeni Mkoa wa Tanga.
Rahma amesema Katibu Mkuu, Ado Shaibu na Katibu wa Ngome ya Wazee, Janeth Fusi, wataongoza kampeni kitaifa kwenye mikoa ya Ruvuma, Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe,” amesema.
Hata hivyo, Rahma amesema Naibu Katibu Mkuu Bara, Ester Thomas, akiambatana na Katibu wa Haki za Binadamu, Mbarala Maharagande wataongoza kwenye mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Mara, Kagera na Geita.
Amesema mbali na misafara hiyo pia kutakuwa na kampeni itakayoongozwa na wajumbe wa kamati kuu, wajumbe wa halmashauri kuu na mawaziri kivuli kwenye mikoa yote ambayo imesalia.
Katika hatua nyingine, amesema chama hicho kimeanza hatua ya kufanya maandalizi muhimu kwa ajili ya kufungua kesi mahakamani kupinga kuondolewa kwa wagombea wao zaidi ya 300 katika uchaguzi huo.
“Ofisi ya Katibu Mkuu imeshakiandikia Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kuomba kuongezewa nguvu ya mawakili kuhakikisha wanafungua kesi dhidi kuenguliwa kwa wagombea wao zaidi ya 3,000,” amesema.