Dk Dimwa: CCM imejipanga uchaguzi Serikali za mitaa

Katavi. Mlezi wa Mkoa wa Katavi na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa, amesema chama hicho kimejipanga kuhakikisha wagombea wake wanashinda katika uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.

Amesisitiza kuwa nguvu ya kidemokrasia na ridhaa ya wananchi ndio itakayoiwezesha kupata ushindi mkubwa.

Dk Dimwa amesema hayo leo Novemba 19,2024 alipokuwa akizungumza na wajumbe wa kamati za siasa za kata, mkoa, na wilaya pamoja na wagombea wateule na wale walioshindwa katika uchaguzi wa kura za maoni katika ukumbi wa Manispaa ya Mpanda mkoani humo. Ziara hiyo ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa 2024.

Mlezi huyo ameeleza kuwa ushindi katika uchaguzi huo utakuwa chimbuko muhimu la kutathmini ushindi wa chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, kwa ngazi za madiwani, wabunge na Rais.

Amesisitiza kuwa chama kina hakika ya kupata ushindi kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025, ikiwamo uimarishaji wa sekta za afya, elimu, kilimo, uvuvi na miundombinu.

Pia, ujenzi wa barabara za kisasa, umeme na huduma za mikopo kwa wajasiriamali wa makundi yote ya kijamii.

Katika hatua nyingine Dk Dimwa pia amekemea makundi yanayoharibu umoja wa chama na kuwataka wanachama kuwa wamoja.

 Amewataka wajumbe wa kamati za siasa kutimiza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya chama na kuhamasisha wananchi wote kuwapigia kura wagombea wa chama hichi, katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

“CCM ni chama kimoja na hatuwezi kuwa na makundi yanayoharibu umoja wetu. Tunapaswa kuwa na mshikamano ili tuweze kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan katika juhudi zake za kuleta maendeleo kwa wananchi. Msingi wa chama chetu ni umoja, na umoja ni nguvu,” amesema Dk Dimwa.

Aidha, Dk Dimwa amewahimiza wagombea wateule kutowadharau wagombea walioshindwa katika uchaguzi wa kura za maoni.

Amesisitiza kuwa kura za maoni ni sehemu ya mchakato na kwamba chama hicho kina nafasi kwa kila mmoja.

“Huu siyo mwisho wa safari yenu ya kisiasa, kura za maoni sio kipimo cha mwisho, bali ni sehemu ya mchakato. CCM ina nafasi kwa kila mmoja, wale walioshindwa wanapaswa kujivunia kwamba waligombea kwa heshima na kuendelea kuwa sehemu ya chama cha Mapinduzi,” amesisitiza.

Amesisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuimarisha chama kwa kuzingatia maadili na kuhakikisha wanatekeleza haki na usawa kwa wanachama wote. Amewapongeza wazee, viongozi watendaji na wanachama wa Mkoa wa Katavi kwa juhudi zao za kuhakikisha chama na jumuiya zake zinaendelea kuimarika kila siku.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Katavi, Idd Kimanta ameeleza kuwa chama hicho kimejipanga  kuhakikisha wagombea wote wanashinda kutokana na mshikamano na umoja baina yao uliopo mkoani humo.

Mwenyekiti wa Wilaya ya Mpanda, Joseph Lwamba amesema licha ya changamoto zilizojitokeza katika uchaguzi wa kura za maoni, wanachama, wagombea wateule, na wale walioshindwa wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanapata ushindi.

Mbunge wa Mpanda, Sebastian Kapufi amesema kuwa maandalizi ya kuhamasisha wanachama na wananchi kujitokeza kupiga kura yanaendelea vizuri, ili kukamilisha ushindi.

Mbunge wa Nsimbo, Anna Lupembe ameeleza kuwa Serikali ya awamu ya sita imefanya kazi kubwa mkoani humo na majimbo yake.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa Sh1.3 trilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika mkoa huo.

Related Posts