Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amewaomba viongozi wa dini mkoani hapa watumie nafasi zao kuhamasisha waumini kujitokeza katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na kuhakikisha amani inatawala.
Amesema ili uchaguzi uende vizuri, uhuru na haki vinapaswa kuzingatiwa lakini lengo kuu likiwa ni kupata viongozi imara ambao ni nguzo muhimu za utatuzi wa kero na kufanikisha maendeleo ya wananchi kuanzia kwenye Serikali za mitaa.
Aidha, Makonda amewaomba viongozi hao kuendelea kumtia moyo Rais Samia Suluhu Hassan akisema kazi za viongozi wa dini ni kuomba kile kisicho sawa ili kikae sawa.
Mkuu huyo wa mkoa amesema hayo leo Jumanne Novemba 19, 2024 alipokuwa akizungumza na viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali Arusha.
Amesema bado viongozi hao wana nafasi kubwa ya kuhamasisha uchaguzi huo ambao kampeni zake zinaanza kesho Jumatano.
“Rais anatambua mchango na nafasi yenu, niwaombe viongozi wangu wa dini, tuhakikishe mchakato huu wa kupata viongozi wetu wa mitaa kuanzia kwenye kampeni mpaka uchaguzi wenyewe, tunakuwa na amani na utulivu,” amesema Makonda.
Amesema siku zote mtaji mkuu wa binadamu ni amani, afya njema na utulivu, nchi inapokosa amani, hata kama ina utajiri wa vivutio vya utalii vya aina gani au madini ambayo hayapatikani mahala popote duniani ni kazi bure.
“Kuna watu husema bora liwalo na liwe, kauli hii haikuwa sawa, bora amani kuliko machafuko. Uchaguzi usiwe chanzo cha kuvuruga amani, tufanye kila jambo kwa kiasi huku tukitanguliza hofu ya Mungu,” amesema Makonda.
Akizungumzia Desemba 9, 2024 Tanzania itakapoadhimisha miaka 63 ya Uhuru, Makonda amesema Mkoa wa Arusha utafanya kongamano maalumu la maombi lenye lengo la kuombea nchi na mkoa huo.
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM), Dk Philemon Mollel amesema wanaishukuru Serikali kwa kuwatambua na kuwashirikisha katika masuala muhimu likiwamo hili la uchaguzi wa Serikali za mitaa.
“Tunashukuru Serikali kwa kutambua mchango wetu na kutushirikisha kwenye masuala muhimu, tutahakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani kwa kutoa ujumbe kwa waumini wetu ili wasifanye vurugu na uchaguzi ufanyike kwa amani,” amesema Dk Mollel.