Mgambo watakiwa kutumika kutunza amani

Songwe. Mkuu wa Wilaya ya Ileje, mkoani Songwe, Farida Mgomi ametoa wito kwa wahitimu wa mafunzo ya Jeshi la Akiba kushiriki katika utunzaji wa amani hususan kipindi hiki cha uchaguzi wa serikali za mitaa.

DC Farida ameyasema hayo Novemba 18, 2024 wakati wa kufunga mafunzo ya Jeshi la Akiba wilayani hapo.

“Tunatarajia kuona mnayatumia vizuri mafunzo haya, na Serikali ya wilaya inawaamini na kuwategemea sana katika kulinda amani na usalama wa nchi,” amesema.

DC Farida amesisitiza juu ya umuhimu wa kutumia mafunzo hayo kuleta mabadiliko chanya katika jamii ikiwemo suala zima la kuwa macho ya Serikali katika kuibua maovu katika jamii lakini pia kutekeleza majukumu wanayopewa na viongozi wao pasina kujali hali.

“Nyinyi sasa ndo mtakuwa macho na masikio kwa serikali kwa kutoa taarifa ya viashiria vibaya vya nchi…msiwe watu wa kufata mkumbo na badala yake muwe wazalendo watiifu, hodari na waadilifu,” amesema.

Pia, amewahakikishia wahitimu hao kuwa Serikali inatambua changamoto zilizopo hususan wakati wa mafunzo hivyo kupitia Ofisi yake changamoto zimepokelewa kama zilivyoainishwa katika risala na kuahidi kufanyiwa kazi ili kuendelea kutambua nafasi ya Jeshi la Akiba katika jamii na Taifa kwa ujumla.

Katika mafunzo hayo kulikuwa na jumla ya wahitimu 174 ambapo wanaume ni 148 na Wanawake 26.

Related Posts