Muheza. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ametoa siku saba kwa mkandarasi anayejenga mradi wa maji wa Miji 28 Wilaya ya Muheza mkoani Tanga kuanza ujenzi wa tenki la eneo la Kilulu baada ya kubaini kuwa ujenzi wake haujaanza.
Agizo hilo amelitoa leo Jumanne Novemba 19, 2024 baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya miradi hiyo wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maji ya Miji 28 inayoendelea mkoani Tanga.
Waziri Aweso ameagiza ndani ya siku saba kama hataona mabadiliko, watumishi wanaosimamia mradi huo sambamba na mkandarasi wote watachukuliwa hatua.
Amemtaka mkandarasi huyo kupeleka vifaa eneo la mradi ndani ya siku hizo na aanze kazi mara moja huku akimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Zainab Abdallah asimamie agizo hilo na kama mkandarasi huyo hatatekeleza, achukue hatua haraka.
“Ninyi mnataka kuzingua, sasa neno ambalo mnataka kulisikia kutoka kwangu ni hili, huu mradi utaondoka na mtu, sijafurahishwa na mwenendo wake, mkuu wa wilaya ninatoa siku saba ujenzi uanze na vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya mradi viletwe haraka ikibidi uchukue hatua,” ameagiza Waziri Aweso.
Awali, mkuu huyo wa wilaya, Zainab alimuomba Waziri Aweso kumchukulia hatua mkandarasi anayejenga mradi huo wa Miji 28.
Amesema mpaka sasa mkandarasi amechimba mashimo tu na hakuna hatua yoyote inayoendelea.
“Hapa Muheza sisi tuna tenki la lita milioni mbili hapa Kilulu tulipo, lakini pia tuna tenki la lita laki tano pale Kwafungo na mradi huu unatarajiwa kuisha mwakani 2025, lakini mimi kama mkuu wa wilaya bado sijaridhishwa na kasi ya utekelezaji wake, tukihoji tunaambiwa tusubiri timu ya Handeni ije kujenga huku Muheza,” amesema Abdallah.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Erasto Mhina amesema baraza la madiwani lilishajadili suala hilo wakiwa na mbunge wakaafikiana watoe agizo kwa mkandarasi, hata hivyo hajatekeleza.
“Kwa hiyo tunakuomba waziri labda wewe uchukue hatua ili ujenzi uanze,” amesema Mhina.
Meneja wa Ruwasa wilayani Muheza, Cleophace Maharangata anayesimamia makandarasi hao, amekiri kutoridhishwa na ujenzi wa matenki hayo na kuahidi mbele ya Waziri Aweso kuwa atahakikisha anasimamia ujenzi huo kwa karibu.
Mradi wa Maji wa Miji 28 Tanga unahusisha wilaya za Handeni, Muheza, Korogwe na Pangani na utagharimu Sh170 bilioni hadi kukamilika kwake.