Fainali ya wanawake mashindano ya klabu bingwa ya mpira wa kikapu nchini ‘betPawa NBL’ itafanyika leo kwa mechi ya DB Lioness na Fox Divers, kwenye Uwanja wa Chinangali, mkoani Dodoma.
Fainali hiyo iliyopangwa kuanza saa 12.00 jioni inatarajiwa kuwa na upinzani mkali kutoka kwa wachezaji wa timu zote mbili.
Fox Divaz ilifuzu fainali hiyo baada ya kuifunga JKT Stars pointi 75- 62, wakati DB Lioness iliichapa Vijana Queens 48-44.
Kabla ya mchezo huo wa fainali kutakuwa na michezo miwili, wa kumsaka mshindi wa tatu kati ya Viipers Queens dhidi ya Orkeeswa, kwenye Uwanja wa Chinangali A na mchezo wa ‘Classification’ kati ya Viipers Queens dhidi ya Orkeeswa Chinangali B.
Washindi kwa upande wa wanaume na wanawake watazawadiwa Sh2.8 milioni wakati washindi wa pili watazawadiwa Sh1.4 milioni.
Fedha hizo zimetolewa na wadhamini wakuu, betPawa na zaidi ya Sh144 milioni zimetengwa kwa ajili ya gharama mbalimbali pamoja na zawadi.
Washindi wa tatu kwa wanawake na wanaume watazawadiwa Sh700,000 na wachezaji bora wa mashindano (MVP) kwa wanawake na wanaume kila mmoja atazawadiwa Sh700,000.
Pia kutakuwa na zawadi ya wafungaji bora, mabeki bora na “best rookie” kwa wanawake na wanaume na watazawadiwa Sh420,000 kila mmoja na zawadi ya ‘sportsmanship kwa wanawake na wanaume itakuwa Sh280,000.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la mpira wa kikapu nchini (TBF), Mwenze Kabinda alisema wanatarajia ushindani mkali katika michezo hiyo ya mwisho na kwani kila timu imeundwa na wachezaji nyota.
“Si unajua kila timu inayoshinda, wachezaji 12 na viongozi wanne wanapewa fedha taslimu, Sh140,000 kutoka kwa wadhamini, wakuu, betPawa. Hadi sasa, wachezaji wote ambao timu zao zimeshinda wamefaidika na kaisi hicho cha fedha,” alisema Kabinda.
Ubora wa Hasheem Thabit kwenye kuzuia ‘blocks’ na kudaka mipira ‘rebound’ uliibeba Dar City iliyoichapa ABC kwa pointi 97-48.
katika mchezo huo, nyota Jshin Brownnlee alifunga pointi 27, na kati ya hizo alifunga mitupo mitatu mara tano, akifuatiwa na Victor Mwoka aliyefunga 15, huku kwa ABC, Elias Shishi alifunga pointi 13, akifuatiwa na Alinani Endrew aliyefunga 11.
Brownlee ndiye kinara wa kufunga pointi nyingi kwenye michuano hiyo baada ya kufunga 135 akiiongoza Dar City hadi fainali.
Brownlee anafuatiwa na Enerico Maengela wa ABC aliyefunga 104, Elias Nshishi wa ABC (90), Tyrone Edward wa UDSM (74) na Soro Geofrey (70).
Walioongoza ufungaji katika maeneo ya mitupo mitatu ‘three points’ ni, Alpha Mchala wa Kisasa Heroes (11), Hussein Juma wa TBT (10), Jshin Brow’nle wa Dar City (9), Sylvian Yunzu wa Outsiders (8) na Felx Luhamba wa JKT (7).
Upande wa ‘asisti’, aliyeongoza ni Gibert Nijimbere wa Dar City (29), Alinani Andrew wa ABC (25), Amini Mkosa wa Dar City (23), Jimmy Brown na Evans Davies wa Outsiders (17).
Katika kuzuia aliyeongoza hadi sasa ni Shishi aliyefanya hivyo mara 17, Hasheem (12), Habibu (11), Tasire Robert wa Outsiders (9), na Moses Jackson wa ABC (7).
Kwa upande wa wanawake aliyeongoza kwa ufungaji ni Noela Renatus wa Vijana Queens (pointi 91), Evelyn Nakiyingu wa Fox Divas (89), Jesca Julias wa JKT (85), Dokouduou Mishele wa Fox Divas (83) na Tumaini Ndossi wa Vijana Queens (80).
Kocha wa UDSM Outsiders alisema hatua ya nusu fainali waliyofikia ni mafanikio makubwa kwani ni mara yao ya kwanza kushiriki mashindano hayo.
Alisema licha ya kufungwa na Dar City kwa pointi 64-54 mchezo wa lakini walipambana na bahati haikuwa upande wao, ingawa ule wa pili vijana wake walicheza na uchovu na kufungwa pia pointi 78-34.
“Kwa kweli bahati haikuwa ya kwetu, ni makosa madogo ndiyo yaliyofanya tupoteze mchezo huo,” alisema Maiga.
Hata hivyo, alisema kwa sasa nguvu yao wanaihamishia kwenye mchezo wa pili wa fainali ya Ligi ya Kikapu Dar es Salaam (BDL) dhidi ya JKT.
Alisema wataingia uwanjani na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wao wa kwanza na timu ya JKT kwa pointi 66-62, na katika mchezo huo watahakikisha hawapotezi tena.