Rais Samia aipongeza Stars, Morocco aweka rekodi

Kocha wa Taifa Stars, Hemed Morocco anaweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kuongoza benchi la ufundi la timu hiyo kuifanukisha kufuzu Michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon).

Morocco ameliongoza benchi la ufundi la timu hiyo leo Jumanne Novemba 19, 2024 kuichapa Guinea bao 1-0 na kuifanya ifuzu michuano hiyo itakayopigwa mwakani nchini Morocco.

Hii ni mara ya nne kwa Stars kufuzu michuano hiyo mikubwa Afrika ambapo mwaka 1980 ilifuzu ikiwa chini ya Mpoland Slawomir Wolk akisaidiana na Joel Bendera, Emanuel Amunike raia wa Nigeria aliipeleka mwaka 2019, huku 2023 ikienda chini ya Adel Amrouche raia wa Algeria.

Wakati huo huo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameipongeza Taifa Stars kwa kufuzu Michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon).

Rais Samia ametoa pongezi hizo katika ukurasa wake wa X (Twitter) akiandika: Tukiwa katika majonzi na kazi ikiendelea katika kuwatafuta ndugu zetu ambao tunaamini bado wako hai kufuatia kuporomoka kwa jengo eneo la Kariakoo, ninawapongeza vijana wetu Taifa Stars kwa ushindi na kufuzu kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025. Mmeandika historia kwa Taifa letu, ikiwa ni mara yetu ya nne kufikia mafanikio haya makubwa katika kipindi cha zaidi ya miaka arobaini.

Hongera kwa kazi nzuri nyote tuliowapa dhamana kusimama na vijana wetu kukamilisha jukumu hili katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), Benchi la Ufundi na Watanzania wote kwa kuendelea kuipenda, kuithamini na kuipa hamasa Timu ya Taifa.

Baada ya ushindi huu, sasa tujikite katika maandalizi mazuri zaidi kwa mashindano yajayo.

Related Posts