Dar es Salaam. Serikali imeifanyia marekebisho Sera ya Taifa ya Ardhi ili kuendana na kasi ya ukuaji wa sekta ya nyumba hapa nchini.
Akizungumza na Mwananchi leo Novemba 19, 2024, Kaimu Mkurugenzi wa Nyumba katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Upendo Matotola amesema kasi ya ukuaji wa soko la majengo nchini umelazimu kuweka udhibiti.
“Kulikuwa na baadhi ya vipengele katika sera ya ardhi ambavyo vilihitaji kuhuishwa na hili tayari limefanyika. Maandalizi yanaendelea ili kuweka sera iliyorekebishwa hadharani,” amesema.
Matotola ameongeza kuwa wizara itaomba idhini ya baraza la mawaziri kabla ya sera hiyo iliyorekebishwa kuwekwa hadharani ili kuandaa sheria mpya ambayo itasimamia sekta ya nyumba nchini.
Sheria mpya, kwa upande wake, itaweka mazingira ya kuanzishwa kwa chombo cha udhibiti cha kusimamia sekta hiyo.
Mapema mwakani, Matotola ameliambia Mwananchi kuwa uamuzi wa kuanzishwa kwa sheria mpya ni kukabiliana na ukuaji wa haraka wa sekta ya nyumba ambayo inastawi kutokana na mazingira mazuri ya biashara yaliyotengenezwa na Serikali.
“Ukuaji huu ni dalili tosha kwamba uchumi wetu unaimarika kwa kasi na tunashuhudia kuongezeka kwa uwekezaji, hasa kwa wawekezaji wa kigeni,” amesema.
Uamuzi wa serikali wa kupitia upya Sera ya Ardhi ya mwaka 2016 unalenga kushughulikia ugumu wa soko la nyumba ambalo limekua kwa haraka katika miaka ya hivi karibuni, Matotola aliongeza.
Maboresho hayo yanafuatia utafiti uliofanywa na wizara, ambayo pia ilibainisha haja ya kuwa na sheria mahususi ya sekta na kutaka kubainisha vipengele muhimu vinavyohitaji kudhibitiwa.
Matotola amesema baadhi ya wadau katika tasnia ya mali isiyohamishika wanatumia fursa ya ukosefu wa udhibiti kuwahadaa wateja na wawekezaji.
“Taarifa sahihi ni muhimu katika mali isiyohamishika kwa kuwa inawawezesha wawekezaji kufanya uamuzi sahihi na kuepuka uwekezaji hatari,” amesema.
Matotola ameongeza kuwa takwimu sahihi na taarifa zinazohusiana zitasababisha uwekaji bei wazi zaidi, kupunguza bei ya juu na kusaidia kupima kwa usahihi mchango wa uchumi wa sekta ya majengo.
Serikali katika miaka ya hivi karibuni imekuwa ikifanya kazi ya kuboresha usimamizi wa mali isiyohamishika kupitia mfululizo wa mipango, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Kitengo cha Majengo ndani ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Julai 2022.
Kitengo hiki kimepewa jukumu la kuratibu na kukuza sekta hiyo, kuhakikisha uwazi wa soko na kukuza mapato ya serikali kutoka kwa sekta hiyo.
Wizara pia imeandaa mikutano kadhaa ya wadau ili kushughulikia masuala muhimu ndani ya sekta hiyo.
“Tunafanyia kazi majukwaa ya kidijitali ili kuhakikisha ufikiaji wa uwazi na rahisi wa habari za sekta ya nyumba,” amesema Matotola.
Wadau wa sekta wameelezea matumaini kuhusu mabadiliko yanayotarajiwa.
Mtendaji Mkuu wa Watumishi Housing Investment (WHI), Fred Msemwa amesema kuanzishwa kwa sheria ya mali isiyohamishika ni muda mrefu.
“Ili maendeleo yatokee katika sekta, tunahitaji kuwa na udhibiti,” amesema.
Hata hivyo, Msemwa ameongeza kuwa sheria ianzishe mamlaka ya uendelezaji wa majengo badala ya mamlaka ya udhibiti ambayo itakuwa ni mdhibiti zaidi kuliko mwezeshaji.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah amenukuliwa akieleza haja ya kuwa na mamlaka itakayosimamia sekta hiyo.
“Mchango wa sekta ya nyumba katika uchumi hauwezi kutekelezwa kikamilifu bila kuwa na chombo sahihi cha kusimamia sekta hiyo. Waendelezaji wanahitaji kuwa na miongozo iliyo wazi wakati wa kupanga miradi,” amesema na kuitaka serikali kuharakisha mchakato wa kutunga sheria mpya ili kuwa na mustakabali wa sekta hiyo.