Siri ya mafanikio ya tuzo za Pmaya yatajwa

Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa uwekezaji bora umeiwezesha Kampuni ya Alaf Limited kushinda Tuzo za Rais kwa Wazalishaji Bora wa Mwaka (Pmaya) kwa miaka 18 mfululizo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Meneja Uhusiano na Mawasiliano, Hawa Bayumi amesema mwaka huu, kampuni hiyo imefanikiwa kupokea tuzo tatu kuu.

Ametaja tuzo hizo kuwa ni muonyeshaji bora katika maonyesho ya TIMExpo2024, mshindi katika sekta ya uzalishaji wa bidhaa za chuma ikiwa ni mara ya 15 mfululizo na mshindi wa pili katika kitengo cha mzalishaji bora wa mwaka wa 2024.

Hafla ya utoaji tuzo hizo ilihudhuriwa na Makamu wa Rais Dk Phillip Mpango aliyeongozana na viongozi wengine wa Serikali na uongozi wa juu wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), ambao ndio waandaaji wakuu wa tuzo hizo hizo zilifanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Hawa amesema tuzo hizo zinatambua kazi nzuri zinazofanywa na wazalishaji mbalimbali nchini Tanzania jambo linalotoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa.

“Malengo ya tuzo hizo ni matatu: kutambua ubora katika viwanda, kuhimiza ubunifu na kukuza ushirikishwaji na kwamba  suala hilo hushirikisha wazalishaji wote walioko hapa nchini,” amesema Hawa.

Pia, amesema Alaf ambayo ni kampuni kongwe hapa nchini, itaendelea kuwa mstari wa mbele kuwa kinara katika kukuza sekta ya ujenzi ili wananchi wapate bidhaa bora zinazoakisi thamani ya fedha wanazotoa wakati wa kununua bidhaa za ujenzi yakiwamo mabati ya kuezekea.

“Katika kuweka msisitizo wa dhamira yetu hiyo, kiwanda chetu cha mabati ya rangi kiko tayari na kinatarajiwa kuanza uzalishaji Desemba mwaka huu; hii ina maana hakutakuwa na haja ya kuagiza mabati yenye rangi nje ya nchi,”amesema.

Hawa amesema wahandisi vijana 30 tayari wamepitia mafunzo ya namna ya kuendesha mtambo huo wa kutengenezea mabati ya rangi na kwamba utaendeshwa na wafanyakazi wa Kitanzania kwa asilimia 100.

Ameushukuru uongozi wa CTI kwa mchango mkubwa kwa kampuni ya Alaf akisema hauna kikomo.

Related Posts