Dar es Salaam. Serikali imesema uongezaji thamani madini nje ya nchi unalikosesha manufaa Taifa, yakiwamo mapato na ajira katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya madini.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema hayo leo Novemba 19, 2024 alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Madini na Uwekezaji uliowakutanisha washiriki zaidi ya 1,500 kutoka ndani na nje ya nchi.
Amesema Serikali inaendelea na mchakato wa kuweka mazingira wezeshi kupitia miongozo, sera, kanuni na sheria katika eneo la uongezaji thamani wa madini.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha sekta ya madini inazidi kuchagia pato la Taifa. Uongezaji thamani ndani ya nchi utaongeza tija. Tanzania ili iweze kufanikiwa zaidi katika sekta ya madini lazima mchakato wa kuongeza thamani madini kufanyika nchini ambapo bidhaa zitokanazo na madini zizalishwe ikiwemo betri za magari na simu kupitia madini ya Kinywe,” amesema.
Amewaomba wawekezaji kuwekeza na kujenga viwanda vikiwamo vya kusafisha madini ya dhahabu kabla ya kusairishwa.
Majaliwa amesema uongezaji thamani madini utaongeza pato la Taifa, ajira, kukuza uwekezaji na kufungua fursa za kibiashara.
Kupitia mkutano huo, amesema watavutia uwekezaji kutoka nje, kuongeza mtaji na teknolojia mpya, kubadilishana maarifa, mawazo na uzoefu, hatua itakayoboresha utendaji wa sekta hiyo.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema Serikali inaenda kumaliza changamoto za wachimbaji wadogo kwa kujenga maabara na ununuzi wa helikopta kwa ajili ya utafiti.
Amesema maabara kubwa ya kisasa ya madini jijini Dodoma na mikoa ya kimadini ya Geita na Chunya zitasaidia kupima sampuli za madini, hatua itakayosaidia wachimbaji waliokuwa wakienda maabara binafsi hadi nje ya nchi kuzipima.
Ukamilishaji wa maabara hizo amesema utakuwa chachu katika ukuaji wa sekta hiyo muhimu katika ukuaji wa uchumi.
Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (Femata), limeiomba Serikali mashine za kuchimba madini, ikieleza kwa sasa ziko 10.
Makamu wa Rais wa Femata, Victor Tesha amesema wanaomba mashine hizo ziwepo kila wilaya nchini.
“Kwa sasa zipo 10, hadi Desemba zinakuja tano, ombi letu tunaomba ziwe nyingi ili kuchochea uchimbaji wa madini na kupata taarifa za kutosha,” amesema.
Pia ameomba leseni maalumu za wachimbaji wadogo akisema: “Tunatambua Serikali kupitia Wizara ya Madini imefuta leseni zaidi ya 2000, tunaomba leseni hizi wapewe wachimbaji wadogo hapa Tanzania.”
Femata imeomba ruzuku ya moja kwa moja kwa vyama vya wachimbaji wadogo ili kuongeza tija ya uchimbaji wa madini.
“Tija itaongezeka ya uchimbaji madini. Tunaunga mkono uongezaji thamani wa madini. Serikali imeanzisha utunzaji wa dhahabu Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tunapongeza hatua hii,” amesema.
Waziri Mkuu Majaliwa akijibu maombi hayo amesema Serikali inaendelea kuyafanyia kazi, ikiwemo kununua mashine za kikanda kisha kwa wilaya na kuwapatia wachimbaji wadogo leseni.
Mkutano huo unalenga kuhimiza umuhimu wa uongezaji thamani wa madini kama njia ya kuleta faida zaidi za kiuchumi na kijamii kwa maendeleo endelevu ya Taifa na dunia.
Pia kupandisha thamani ya madini yanayozalishwa nchini kabla ya kusafirishwa nje kwa lengo la kuchochea uanzishwaji viwanda vitakavyokuwa na manufaa nchini na kwa mataifa jirani.