Urusi yapinga azimio la kusitisha mapigano Sudan – DW – 19.11.2024

Tangu Aprili mwaka 2023, kunaendelea vita nchini Sudan kati ya majenerali wawili wanaohasimiana.

Rasimu ya azimio hilo iliyoandaliwa na Uingereza na Sierra Leone, ilikuwa imetoa wito kwa pande zote mbili kusitisha mara moja uhasama na kuanza mazungumzo katika dhamira ya kufikiwa kwa makubaliano ya usitishwaji mapigano.

Akiongoza  kikao cha baraza hilo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifamjini New York-Marekani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Lammy ameutaja uamuzi huo wa Urusi kuwa ni “fedheha”.

Hayo yakijiri, mjumbe maalum wa Marekani kwa Sudan Tom Perriello amesafiri jana kuelekea Sudan na amekutana na mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan. Ziara hiyo ya Perriello ni yenye lengo la kusaka amani pamoja na ongezeko la misaada kwa mamilioni ya watu wenye uhitaji.

Wanamgambo wa RSF wapinga kukiuka haki na kupewa silaha na UAE

Wanajeshi wa Sudan wakiwa katika doria mjini Khartoum
Wanajeshi wa Sudan wakiwa katika doria mjini Khartoum: Novemba 3, 2024Picha: Amaury Falt-Brown/AFP

Wanamgambo wa Sudan RSF, wamekanusha madai dhidi yao ya kuhusika na ukiukwaji wa haki za binadamu. Kikosi hicho ambacho kimekuwa kikipambana na jeshi la nchi, kwa miezi 19 sasa, kimesema kimejitolea kuleta amani.

Wakizungumza na waandishi habari mjini Nairobi Kenya, wajumbe wa RSF wamekanusha ripoti zilizosambaa kwamba wamepata silaha kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu. Mkuu wa ujumbe huo Jenerali Omar Hamdan Ahmed, amesema hawapati msaada wowote kutoka nchi yoyote.

Soma pia: Watafiti wasema huenda vifo Sudan ni vingi zaidi ya vinavyoripotiwa

Badala yake ameishutumu Misri kwa usaidizi wake mkubwa kwa jeshi la Sudan linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, madai ambayo Misri imekanusha.
Sudan imekuwa katika vita tangu Aprili 2023 kati ya jeshi la nchi na kikosi cha RSF.
Pande zote zimelaumiwa kwa kufanya uhalifu wa kivita ikiwemo kuwashambulia rai ana uporaji.

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamesema RSF na wanamgambo washirika wake wa Kiarabu kwamba katika mji wa El-Geneina pekee magharibi mwa Darfur, wameua kati ya watu 10,000 hadi 15,000.

Vyanzo: ( DPAE, AP, AFP)

 

Related Posts