Washauri mfumo wa elimu unaohimili majanga Afrika

Dar es Salaam. Wakati mataifa mbalimbali barani Afrika yakiendelea kufanya uwekezaji katika sekta ya elimu, wito umetolewa kwa nchi hizo kuweka mifumo itakayofanya elimu iendelee kutolewa hata yatakapotokea majanga.

Wito huo umetolewa na wadau wakati wa mkutano wa kimataifa wa ubora wa elimu ulioandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) uliofanyika Novemba 12 hadi 14 jijini Dar es Salaam ukihusisha washiriki kutoka mataifa ya 16 ya Afrika.

Hoja hiyo imetolewa kuweka msisitizo wa uwekezaji katika mifumo itakayoondoa vikwazo pale yanapotokea majanga ikiwemo mafuriko, magonjwa ya mlipuko na changamoto nyingine zinazoweza kuzuia wanafunzi kusoma.

Mshauri mwelekezi katika masuala ya elimu kutoka shirika la Hakielimu Dk Wilberfoce Meena, anasema kwa miaka ya karibuni kumekuwa na mabadiliko yanayojitokeza katika mifumo ya elimu yakisababishwa na majanga mbalimbali hivyo ni muhimu kwa nchi kuwa na hatua za tahadhari.

Akitolea mfano wa mlipuko wa Uviko 19, mafuriko na matokeo mengine ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa, yamekuwa yakidhoofisha utoaji wa elimu na wakati mwingine kusitisha kabisa shughuli za elimu.

“Hili ndilo limetufanya tukutane hapa kwa pamoja tukibadilishana uzoefu na wenzetu wa mataifa mengine wanafanya nini, lengo likiwa ni kutengeneza mifumo ambayo itawezesha uthabiti wa elimu. Isitokee kwa namna yoyote kwamba majanga yazuie utoaji wa elimu.

“Tunahitaji kuwa na mfumo thabiti wa elimu ambao unaweza kukabiliana na mabadiliko yoyote yanayoweza kutokea na kuathiri utoaji wa elimu. Hapa ndipo tunapoona umuhimu wa matumizi ya teknolojia na si hilo tu tunatakiwa kujipanga kwa namna yoyote ile kuhakikisha utoaji wa elimu haukutani na vikwazo,” anasema Dk Meena.

Kwa upande wake, Mratibu wa TEN/MET Martha Makala anasema imefika wakati ni muhimu kwa nchi kuhakikisha ina mifumo bora, imara na thabiti ya elimu ambayo itafanya elimu iweze kutolewa zaidi ya darasani.

“Tunataka kuwa na mifumo iweze kutoa elimu hata nje ya darasa, tumeshahuhudia majanga kama magonjwa ya mlipuko, matetemeko ya ardhi, mvua zinazosababisha mafuriko, tunapaswa kujiuliza je mifumo tuliyonayo inawezesha wanafunzi kuendelea kusoma yakitokea hayo.

“Zipo nchi ambazo zimepiga hatua katika eneo hilo ndiyo maana tumekutana kwa pamoja tushirikishane uzoefu katika kujenga mifumo bora na thabiti katika kuhakikisha tunatoa elimu iliyo bora, jumuishi na inapatikana kwa watu wote,” anasema Martha na kuongeza.

“Kufanikisha hilo tutakuwa na mijadala mbalimbali ikiwemo uwekezaji wa rasilimali za ndani katika kusaidia na kuboresha sekta ya elimu, Tanzania tupo kwenye mageuzi ya kisera na mitaala na mwaka 2028 tutashuhudia wanafunzi wa makundi mawili wakiingia kidato cha kwanza kwa maana wale watakaoishia darasa la sita na wale watakaomaliza darasa la saba mwaka 2027 hivyo ni lazima tujiandae,”.

Katika kongamano hilo, Waziri wa Elimu, Sayansi, na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda, alisisitiza dhamira ya Serikali katika mabadiliko ya elimu.

“Tunahitaji kuhakikisha tunazalisha wahitimu wenye ujuzi. Safari hii inaweza isiwe rahisi, lakini ikiwa tutaendelea na malengo yetu, elimu yetu itakuwa na manufaa makubwa,” alisisitiza.

 Profesa Mkenda anaeleza kuwa Tanzania tayari imeanzisha mtalaa mpya unaolenga kuwapatia wanafunzi ujuzi wa vitendo, hasa kupitia mafunzo ya ufundi, ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira.

Kongamano hilo pia lilihimiza kuchunguza mifumo mipya ya ufadhili, ikijumuisha ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi na ukusanyaji wa rasilimali za ndani.

 Washiriki wanasema kuwa ushirikiano huu ungeweza kutoa njia endelevu ya kuongeza fedha kwa elimu huku ukitumia nguvu za sekta mbalimbali.

Eneo lingine muhimu lililozungumziwa ni kupunguza pengo la kidijitali ambapo Martha anasema: “Ujuzi wa kidijitali ni muhimu katika elimu ya kisasa, na kushughulikia pengo la kidijitali kutahakikisha mazingira ya kujifunzia ni ya kujumuisha na yenye ufanisi.”

Akizungumia hilo Profesa Mkenda alisisitiza dhamira ya Serikali katika kujumuisha ujuzi wa kidijitali katika mtalaa, akieleza kuwa ustadi wa kiteknolojia ni muhimu ili wanafunzi waweze kufanikiwa katika soko la ajira linalobadilika kila siku.

“Kwa kuingiza mafunzo ya ujuzi wa kidijitali katika elimu ya sekondari, Tanzania inatarajia kuwajengea wanafunzi ujuzi muhimu kwa ajili ya ajira katika zama za kidijitali,” anasema.

 Kongamano hilo lilionyesha haja ya dharura ya mifumo ya elimu inayojumuisha makundi yaliyotengwa, ikiwa ni pamoja na wasichana, watoto kutoka familia maskini, watoto wenye ulemavu, na wale walioko katika maeneo ya mgogoro au dharura.

“Elimu jumuishi siyo tu kuhusu kuandikisha wanafunzi wote; ni kuhusu kubuni mifumo inayowezesha na kusaidia mahitaji yao mbalimbali,” anaeleza Martha.

 Wengi walikubaliana kuwa aina hii ya ujumuishaji itawawezesha wanafunzi wengi kushiriki kikamilifu katika elimu na kupata njia za kufikia maisha bora.

Mbali na kuboresha miundombinu, azimio lilisisitiza umuhimu wa elimu ya mazingira kuwa sehemu muhimu ya mtalaa wa Afrika, ili kuwajengea wanafunzi ufahamu wa changamoto za kimazingira zinazokabili jamii zao.

 Kwa kuendelea mbele, washirika wanatarajiwa kuunganisha juhudi zao na mkazo wa serikali katika kukuza ujuzi, ufadhili na sera jumuishi.

Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917.

Related Posts