Dar/Mikoani. Ikiwa ni siku ya kwanza za kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa jana, baadhi ya vyama vya siasa vimezindua kampeni zao, huku vyama vingine vikipanga kuanza leo kuelekea siku ya uchaguzi huo, Novemba 27, mwaka huu.
Katika uchaguzi huo utakaohusisha nafasi za wenyeviti na wajumbe wa mitaa, vijiji na vitongoji kote nchini, wagombea kupitia vyama vyao wanakwenda kuzungumza na wananchi wakinadi sera na vipaumbele vyao.
Wakati viongozi wakuu na wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM wakitawanyika katika mikoa mbalimbali nchini, viongozi wa vyama vya upinzani nao wametawanyika katika maeneo tofauti kusaka kura, ili wapate ushindi kwenye uchaguzi huo.
Katika kusaka kura hizo, baadhi vinatumia staili tofauti, ikiwemo kuwatumia viongozi wa maeneo husika kuwanadi na kuwaomba kura wagombea wao, wakati wengine wakiwatumia viongozi wao waandamizi.
Viongozi wa vyama hivyo walitoa ujumbe kwa wananchi wakiwataka kuchagua wagombea wao ili watatue changamoto zinazowakabili kwenye maeneo yao, huku wengine wakijivunia kazi walizozifanya miaka mitano iliyopita.
ACT na ahadi kwa wananchi
Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu alizindua kampeni za chama chake mkoani Pwani huku akiwataka wananchi wa mkoa huo kukiunga mkono chama hicho katika uchaguzi huo, akisema ndicho chama chenye majibu ya changamoto zinazowakabili.
Semu ameeleza hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Kazole, kilichopo Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa kampeni za chama hicho.
“ACT Wazalendo tuna viongozi bora na thabiti, wanaopinga rushwa na kuheshimu utawala wa sheria kwa kushirikisha wananchi katika mipango ya maendeleo, ikiwemo kila fedha inayoletwa, inatumika katika mipango husika.
“Tutahakikisha viongozi wetu wanasimamia matumizi bora ya ardhi, kwa sababu Pwani ina changamoto kubwa ya migogoro ya ardhi, tutakwenda kulitimiza hili, sambamba na kusimamia ahadi yetu ya kwamba kiongozi wa ACT anayejihusisha na rushwa tutamuondoa,” amesema.
Mbali na hilo, Semu amewasihi wananchi wa Pwani kutumia haki yao ya msingi kuchagua viongozi bora watakaowaletea maendeleo katika kipindi cha miaka mitano ijayo, huku akiwataka kutowachagua viongozi wasiotekeleza majukumu yao.
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria, Ezekiah Wenje amesema licha ya idadi kubwa (bila kutaja idadi) ya wagombea wa chama hicho kuenguliwa, Chadema itahakikisha waliopitishwa wanashinda.
“Leo (jana) tumefungua kampeni kila mahali katika kanda yetu, mimi nimefanya mikutano katika kata nane za Jiji la Mwanza, tutaendelea kuwanadi wagombea wetu kila mahali hadi nyumba kwa nyumba,” amesema Wenje.
Kuhusiana na maeneo ambayo hakuna wagombea wa Chadema, Wenje amesema wagombea wa chama hicho watahamasisha wagombea wa vyama vingine kupiga kura ya hapana kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi huo.
Katibu Mkuu wa Chadema, Kanda ya Magharibi, Meshack Micus amesema chama chake kimezindua kampeni kwenye wilaya tatu ambazo ni Urambo, Igunga pamoja na Sikonge, huku wilaya nyingine wakitarajia kufanya uzinduzi baada ya Novemba 20, 2024.
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Mkoa wa Mwanza, Ramadhani Amrani amewataka wananchi kuchagua viongozi wanaowataka, hasa wa chama hicho kwa kuwa wana siasa za kistaarabu.
Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi alizindua kampeni za chama hicho mkoani Mwanza, ambapo aliwapiga kijembe wapinzani, akisema japo walikuwa wanawabembeleza wanachama wao kugombea, wameishia kupata wagombea 20,000 katika vitongoji zaidi ya 60,000 na wagombea 5,000 katika vijiji zaidi ya 12,000.
“Nitumie nafasi hii kuwataka wagombea wetu walioteuliwa kuilinda na kuienzi heshima kubwa ambayo CCM inapewa na Watanzania. Tunaamini kuwa mtachaguliwa lakini tunawasihi mkajiepushe na dhuluma, rushwa, mkatumie nguvu zenu kuwatumikia Watanzania ili kuongeza imani yao kwa uongozi wenu,” amesema.
Akizindua kampeni za CCM mkoani Mbeya, Naibu Katibu Mkuu chama hicho (Bara), John Mongella amesema hawafurahishwi na migogoro inayoendelea kwa vyama vya upinzani (Chadema) ambayo imewafanya wamshindwa kuweka wagombea baadhi ya maeneo.
“Wakati tunawaombea wawe imara, lazima maendeleo yaendelee, tuwachague wagombea wa CCM, wale wengine bado hawajakomaa na mtoto akimaliza shule huwezi kumpa mke lazima ujiridhishe amekomaa,” alisema Mongella.
Huko Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amezindua kampeni hizo kimkoa huku akitaja sababu tatu za kwa nini Watanzania wanapaswa kuwachagua wagombea wa chama hicho.
Sababu hizo ni pamoja na kwamba CCM ndiyo inayotekeleza ilani ya uchaguzi 2020/25, mafanikio ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo ni matokeo ya wa ushirikiano na viongozi wa Serikali za mitaa, vijiji, vitongoji, madiwani na wabunge.
Sababu nyingine alisema ni tamko kuhusu uchaguzi huo na mambo ya kuzingatia pamoja na chama hicho kuwa na dhamana na wajibu wa kuwatumikia Watanzania.
“Licha ya changamoto ndogondogo zilizopo, lakini mafanikio yapo, hakuna miradi iliyotekelezwa ya ujenzi wa madarasa, pasipo ushirikiano wa serikali za mitaa.
“Kama tulifanikiwa kufanya kazi na watu hawa (viongozi wanaomaliza muda wao) basi CCM imewaletea tena watu sahihi, tunaomba muamini wabunge na madiwani watafanya nao kazi vizuri,” amesema Makalla.
Huko Katavi, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa amewaomba wananchi kuweka mbele maslahi ya maendeleo yao kwa kuwachagua wagombea wote wa CCM katika uchaguzi ujao.
“Wito wangu kwenu wananchi wote katika kata zote 58 zilizopo katika mkoa huu, jitokezeni Novemba 27, 2024 mkawapigie kura nyingi wagombea wote wa CCM ili wakatekeleze mahitaji yenu kwa vitendo,” amesema Dimwa.
Katibu Mkuu wa DP, Abdul Mluya amesema chama hicho, kitazindua kampeni zake kitaifa leo mkoani Kigoma ambako wana msingi mzuri wa wagombea wao.
“Nitazindua mwenyewe kampeni hizi, nitakwenda pia Tabora, Kahama na Mara, katika uchaguzi wa mwaka 2014, tulifanikiwa kupata viti vya vitongoji na vijiji mkoani Kigoma, sasa tunataka tukavitetee,” amesema Mluya.
Kwa mujibu wa Mluya, maofisa wengine waandamizi wa DP, wakiwemo wakurugenzi, wajumbe wa halmashauri kuu ya chama hicho, wamegawanywa katika maeneo ya kimkakati ambayo DP imesimamisha wagombea.
Kwa upande wao, Chama cha Sauti ya Umma (Sau) kinatarajia kuzindua kampeni zake za uchaguzi wa Serikali za mitaa kesho Novemba 21, 2024 katika Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Majaliwa Kyara amesema wameweka wagombea 307 watakaogombea uenyekiti wa serikali za mitaa nchi nzima ambapo wanatarajia kuzindua kampeni hizo mkoani Tanga.
“Watakapozindua kampeni hizo ni viongozi wa kitaifa wakiongozwa na Mwenyekiti wa Sau na tukishazindua tutajigawa, wengine wataenda Kilimanjaro, Arusha, Manyara Dodoma, Mwanza, Mara huku wengine wakienda Pwani, Dar es Salaam na Morogoro,” amesema Kyara.
Wilaya za kichama zapewa jukumu
Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma wa Chama cha Wananchi (CUF), Mohamed Ngulangwa amesema utaratibu wa chama hicho, kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa zinasimamiwa na viongozi wao wilaya.
“Tunatumia viongozi wetu wa wilaya na kata, tofauti na kampeni za uchaguzi mkuu ambazo kuna maofisa kutoka makao makuu ya chama wanakwenda kuwanadi wagombea,” amesema Ngulangwa.
Mwenyekiti wa Ada Tadea, Juma Ali Khatib ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, amesema kampeni za mchakato huo, zinasimamiwa na viongozi wa ngazi husika zikiwemo wilaya na mikoa, kulingana na uwezo wao.
“Hatuwezi kushinda wenzetu, hatuna rasilimali za kutosha kupeleka viongozi wakuu kila mahali, ingawa mimi kesho (Alhamisi) nitakwenda Kilombero (Morogoro), wakati katibu mkuu wangu akienda Maswa na Simiyu,” amesema Khatib.