Ahukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kumbaka mtoto wa miaka minane

Mwanza. Mahakama ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, imemhukumu Samwel Anthony (34) kifungo cha maisha jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto wa miaka minane.

Anthony ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Shirima wilayani Kwimba mkoani humo, ametenda kosa hilo Agosti 16, 2024.

Hukumu ya Anthony imetolewa baada ya Mahakama kuwasikiliza mashahidi watano wa Jamhuri, akiwamo mwathiriwa wa ukatili huo (jina linahifadhiwa) na kujiridhisha kwamba alitenda kosa hilo.

Wakati wa kumsomea maelezo ya awali katika shauri hilo la jinai namba 24025/2024, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Juma Kiparo aliieleza Mahakama kuwa mwathiriwa alitendewa kitendo hicho na Anthony alipokuwa akitoka dukani kununua mahitaji aliyoagizwa na mama yake.

“Mwathiriwa alitendewa kitendo hicho wakati ameagizwa na mama yake dukani na wakati anarudi ndipo Samwel alimvuta nyuma ya nyumba yake kisha kumfanyia ukatili huo,” amesema Kiparo.

Kwa mujibu wa Kiparo, mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 130 (1)(2)(e) na 131 (3) cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16, Marejeo ya mwaka 2022.

Baada ya kusomewa maelezo ya awali, mshtakiwa alikiri kutenda kosa hilo na kuiomba Mahakama kumpunguzia adhabu kwa kile alichodai anasumbuliwa na tatizo la mapafu na anategemewa na watoto watano akiwamo mmoja mwenye ulemavu wa viungo.

“Mheshimiwa naomba kupunguziwa adhabu kwa sababu mimi ni mgonjwa wa mapafu, pia nina watoto watano mmoja mlemavu, wote wananitegemea, nina mdogo wangu ambaye ninamlea ni mgonjwa…mke wangu nitamuachia mzigo mkubwa kuilea hiyo familia,” amesema Anthony.

Hakimu Mkuu wa Mahakama hiyo, Dastan Ndeko ametoa hukumu ya kifungo cha maisha jela kwa Anthony, leo Jumatano Novemba 20.

“Mshtakiwa (Anthony) Mahakama hii imekutia hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto mdogo wa miaka minane kinyume cha sheria. Hivyo, inakuhukumu kutumikia kifungo cha maisha jela,” amesema Hakimu Ndeko.

Baada ya kuhukumiwa kifungo hicho, Anthony amechukuliwa na maofisa wa Jeshi la polisi kupelekwa gerezani kwa ajili ya kuanza kutumikia kifungo chake.

Related Posts