Askofu Kassala: Serikali izitazame changamoto za watoto wenye ulemavu

Geita. Askofu wa Jimbo Katoliki Geita, Dk Flavian Kassala ameitaka Serikali kuziangalia na kuzitatua changamoto zinazowakabili watoto wenye ulemavu zinazowafanya kukosa elimu kama watoto wengine.

Askofu Kassala ameyasema hayo Novemba 19, 2024 wakati akikabidhi vifaa mbalimbali vya kujifunzia, michezo na vya kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu katika kituo cha elimu maalumu Mbugani mkoani hapa, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kuondoa imani potofu dhidi ya watoto wenye ulemavu.

Mradi huo unatekelezwa na Kanisa Katoliki kwa kushirikiana na mgodi wa dhahabu wa Geita (GGML) kwa ufadhili wa World Gold Council.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Askofu Kassala amebainisha changamoto zinazowakabili watoto hao kuwa ni pamoja na gharama kubwa za vifaa vya kujifunzia na kufundishia, ukosefu wa vifaa maalumu vya kutumia watu wenye ulemavu na ugumu wa kupata mikopo ya elimu ya juu kwa watu wenye nia ya kusoma fani ya elimu maalumu.

Askofu Kassala amesema watoto wengi wenye tatizo la ulemavu wanakosa fursa mbalimbali za kijamii ikiwemo elimu, kutokana na changamoto zinazowakabili.

“Ukienda dukani kununua fimbo ya mtu asiyeona, ni gharama kubwa, hata vifaa vya kutolea elimu maalumu ni gharama, lakini hata kuzipata ni changamoto na kwa upande mwingine hata wataalamu hasa walimu ni wachache na haya yanafanyika wakati taasisi za kutoa elimu hizo zipo,” amesema.

Amesema wanaotaka kwenda kujifunza elimu ya kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu wanakutana na changamoto ya mikopo na kushindwa kusoma, hivyo ameishauri Serikali kuweka kipaumbele kwenye sekta ya elimu maalumu kwa kuwalipia ada kama motisha ya kusomea elimu maalumu.

 “Wataalamu ni wachache wakati taasisi za kuwaandaa wataalamu hao zipo, wengi wanakwama kutokana na gharama za ada na wanakosa mkopo na hivyo kushindwa kwenda kusoma ili warudi kujitolea kuwahudumia hawa wengine. Na hata wakipewa mkopo wanadaiwa sawa na hawa wenye hali ya kawaida, Serikali inapaswa ilitazame hili,” amesema.

Awali, akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Ofisa Elimu ya Watu Wazima mkoani humo, Salome Cherehani amesema idadi ya walimu waliopo wa elimu maalumu haiendani na wingi wa wanafunzi.

Amesema Mkoa wa Geita wenye walimu 146 wa elimu maalumu una wanafunzi 3,644, kati yao 1,845 wapo kwenye vituo maalumu vya elimu na 1,799 wapo kwenye shule jumuishi, idadi ambayo haiendani na wingi wa walimu.

“Mfano wenye usonji, mwalimu mmoja anapaswa afundishe mwanafunzi mmoja, wale wenye shida ya akili, mwalimu mmoja wanafunzi watano hadi saba, kwa wale viziwi na wasioona mwalimu mmoja wanafunzi 12, lakini kutokana na upungufu, unakuta mwalimu mmoja anahangaika na makundi yote,” amesema Cherehani.

Kaimu Meneja wa mgodi wa GGML, Elibariki Jambau amesema mgodi huo umejikita kushughulikia changamoto mbalimbali za kijamii ikiwemo zinazowakabili watoto wenye ulemavu.

Amesema dhamira yao ni zaidi ya shughuli za uchimbaji madini na kwamba wamejikita kusaidia makundi yaliyo kwenye mazingira magumu na kukuza maendeleo endelevu.

VVifaa vilivyotolewa ikiwemo miwani ya albino, kamusi za lugha ya alama, viti mwendo na vifaa vingine, ni kuonyesha kile kinachoweza kufanyika pale wadau wanapokuwa na lengo moja,” amesema Jambau.

Mratibu wa mradi wa kuondoa imani potofu kwa watoto wenye ulemavu mkoani Geita, Joseph Massawe amesema mradi huo ulioanza Februari 2023, unalenga kuwajengea wazazi na jamii uwezo wa kuelewa na kutambua kuwa mtoto mwenye ulemavu ni sawa na mwingine.

Amesema mradi huo ambao umelenga kutambua aina za ulemavu walionao watoto, umefanikisha kuwatambua 5,216 na kubaini mahitaji yanayowakabili.

Related Posts