Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda, Dk Kizza Besigye anadaiwa kutekwa na watu wasiojulikana jijini Nairobi, Kenya.
Kwa mujibu wa tovuti ya Daily Monitor ya nchini Uganda, Dk Besigye ambaye ni mpinzani wa muda mrefu wa Rais Yoweri Museven aliripotiwa kutekwa Jumamosi Novemba 16, 2024 jijini Nairobi alipokwenda kuhudhuria uzinduzi wa kitabu cha mwanasiasa wa Kenya, Martha Karua.
Taarifa zilizochapishwa na Daily Monitor zinadai mara ya mwisho Dk Besigye alionekana katika ghorofa moja Mtaa wa Riverside, Westlands nchini Kenya.
“Dk Besigye aliwaambia washirika wake kwamba alikuwa anaenda kukutana na mtu ambaye hajafahamika katika ghorofa hiyo na alishushwa hapo na dereva wa teksi ambaye alibaki anamsubiri.
“Hata hivyo, dereva aliondoka baada ya kusubiri kwa saa kadhaa bila Dk Besigye kurejea,” imeripoti tovuti hiyo.
Hata hivyo, mkewe Winnie Byanyima amedai kuwa mume wake anashikiliwa katika gereza moja la kijeshi nchini Uganda.
“Ninaiomba serikali ya Uganda kumwachilia mume wangu Dk Kizza Besigye kutoka mahali anapozuiliwa mara moja. Alitekwa nyara Jumamosi alipokuwa Nairobi kwa ajili ya uzinduzi wa vitabu vya Martha Karua. Sasa nimearifiwa kwa uhakika kwamba yuko katika jela ya kijeshi huko Kampala,” ameandika Winnie ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa UNAIDs nchini Uganda.