Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetupilia mbali ombi la kuzuia dhamana ya mshtakiwa Ferdnand Ndikuriyo (27), maarufu Chuma cha Chuma, lililowasilishwa na Serikali.
Mahakama imempa masharti ya dhamana mshtakiwa huyo, ambaye ni msanii wa muziki na raia wa Burundi anayekabiliwa na shtaka moja la kuwepo nchini Tanzania bila kibali.
Uamuzi huo umetolewa leo Novemba 19, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga baada ya kupitia maombi yaliyowasilishwa na upande wa mashtaka na ule utetezi kuhusu kuzuia dhamana ya mshtakiwa huyo.
Hakimu Ruboroga ametoa masharti matano ya dhamana dhidi ya mshtakiwa huyo ambayo ni mshtakiwa kusaini bondi ya Sh10 milioni.
Kuwa na wadhamini wawili wanaotambulika kisheria na wawe raia wa Tanzania watakaosaini bondi ya Sh10 milioni kila mmoja.
Mshtakiwa anatakiwa kuwasilisha fedha taslimu Sh20 milioni au mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.
Masharti mengine ni mshtakiwa kusalimisha hati ya kusafiria na nyaraka nyingine muhimu na hatakiwi kusafiri nje ya Mkoa wa Dar es Salama bila ruhusa ya Mahakama.
Mshtakiwa ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana, hivyo amerudishwa rumande.
Awali, akisoma uamuzi kuhusu dhamana, Ruboroga amesema upande wa mashtaka uliwasilisha maombi kuzuia dhamana ya mshtakiwa huyo ukiainisha sababu nne.
Maombi hayo yaliwasilishwa Novemba 8, 2024 na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema akishirikiana na Rapahel Mpuya, ambapo waliomba mahakama isitoe dhamana kwa kuwa mshtakiwa hajulikani anaishi wapi kwa sababu hana anuani ya makazi aliyoiwasilisha mahakamani, mshtakiwa si raia wa Tanzania, na alishatoa taarifa kuwa anatishiwa usalama wake.
Sababu nyingine, walidai kwa taarifa za uchunguzi wa awali wamejulishwa vyombo vya uchunguzi vimepokea taarifa kuwa nchini kwake anatuhuma nyingine za makosa ambayo bado hawajawasilisha rasmi.
Upande wa mashtaka ulidai kupewa kwake dhamana kunaweza kusababisha mshtakiwa kutumia nafasi hiyo kutoroka.
Mawakili hao walidai kutokana na sababu hizo, upande wa mashtaka unaomba Mahakama izuie dhamana ili kumlinda mshtakiwa asidhurike wakati kesi ikiendelea mahakamani.
Wakili wa mshtakiwa, Hery Kimaro alidai pingamizi hilo si la kisheria na haliwezi kuzuia mshtakiwa asipewe dhamana kwa sababu ana mke na watoto nchini.
Wakili Kimaro alidai kuhusu hoja za kutishiwa usalama wake hazina uthibitisho, hivyo aliomba Mahakama impatie dhamana.
Hakimu Ruboroga baada ya kupitia hoja za pande zote, amesema licha ya hoja ya za upande wa mashtaka kuwa na mashiko, lakini mshtakiwa ana haki ya kupewa dhamana kama ambavyo upande wa mashtaka walisema katika maombi yao, wakieleza iwapo Mahakama itatoa dhamana basi apewe masharti magumu.
Baada ya kutoa uamuzi, hakimu alitaja masharti ya dhamana ambayo mshtakiwa ameshindwa kuyatimiza na kurudishwa rumande.
Kesi imeahirishwa hadi kesho, Novemba 20, 2024 kwa ajili ya usikilizwaji wa kesi ya msingi.
Katika shauri la msingi, Chuma ambaye makazi yake ya muda ni Mbezi Luis anadaiwa kutenda kosa hilo Septemba 18, 2024 eneo la Upanga, Las Vegas Casino, Ilala, Dar es Salaam.
Anadaiwa akiwa eneo hilo alibainika kuwepo nchini bila kuwa na kibali, wakati akijua kuwa ni kinyume cha sheria.
Kwa mara ya kwanza mshtakiwa alifikishwa mahakamani hapo Novemba 5, 2024 na kusomewa kesi ya jinai namba 31005/2024.
Baada ya kusomewa shtaka alikana kutenda kosa hilo.