Derick anayetuhumiwa kujeruhi Club 1245 kupanda kizimbani leo

Dar es Salaam. Derick Junior (36), ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) anayekabiliwa na mashtaka mawili ya kujeruhi katika eneo la starehe la Club 1245, Masaki Dar es Salaam, leo Novemba 20, 2024 atasomewa hoja za awali za kesi inayomkabili.

Mshtakiwa huyo atasomewa hoja hizo wakati wa usikilizwaji wa awali wa shauri hilo katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni.

Katika kesi ya jinai inayomkabili, Derick anadaiwa kujeruhi na la pili kutembea na silaha hadharani kwa namna ya kuleta tishio kwa mtu.

Mshtakiwa alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Oktoba 29, 2024 na kusomewa mashtaka hayo na Wakili wa Serikali, Dickson Swai, mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Is-haq Kupa.

Wakili Swai alidai mshtakiwa alitenda makosa hayo Oktoba 27, 2024 saa 12:30 asubuhi eneo la Masaki katika Club 1245, wilayani Kinondoni.

Anadaiwa katika shtaka la kwanza alimjeruhi Julian Bujuru kwa kumpiga kwa kitako cha bastola na kumjeruhi usoni sehemu ya jicho na puani.

Katika shtaka la pili, anadaiwa tarehe hiyohiyo katika eneo hilo alitoa silaha na kumtishia Bujuru, kitendo ambacho kinatishia amani kinyume cha kifungu cha 84 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Baada ya kusomewa mashtaka, mshtakiwa alikana kutenda makosa hayo na Mahakama ilimpa dhamana.

Related Posts