Job afichua mbinu walizotumia kumzuia Guirassy

HAIKUWA kazi rahisi kwa safu ya ulinzi ya Taifa Stars iliyoongozwa na mabeki wa kati, Dickson Job na Ibrahim Bacca kumzuia mshambuliaji tegemeo wa Guinea na Klabu ya Borussia Dortmund, Serhou Guirassy ambaye amewatesa mabeki wengi katika mechi za kufuzu Afcon 2025.

Jana Jumanne Novemba 19, 2024, Guirassy alikutana na walinzi hao wa Taifa Stars ambao walihakikisha mshambuliaji huyo haleti madhara, wakafanikiwa.

Guirassy ambaye kwenye mchezo wa jana aliingia akiwa na rekodi ya kufunga mabao sita katika mechi tatu zilizopita za kufuzu Afcon 2025 ikiwemo hat trick dhidi ya Ethiopia, mbele ya Stars aliondoka bila ya kupiga shuti lililolenga lango.

Akizungumza na Mwanaspoti, Job alisema walifanikiwa kumsoma staa huyo na kufahamu namna nzuri ya kumzuia ni kuziba nafasi za yeye kupatiwa mipira.

Job aliongeza kuwa, na hata wakati ambao alifanikiwa kupata mpira, walifika haraka kumzuia asilete madhara, ikawa rahisi kwao kumkaba.

“Tulifanikiwa kumkazia kila eneo hadi alipojaribu kupiga krosi tulihakikisha tupo nae bega kwa bega kwani tulifahamu jicho la Guinea liko pale.

“Haukuwa mchezo mwepesi ila tumeweza kufanya vizuri kwa kushirikiana safu nzima ya ulinzi, tulijipanga kuzima mashambulizi yote ili tu kuhakikisha hawapati nafasi, tunafuraha sana kushinda kwani mipango imekwenda sawa,” alisema Job.

Stars imefuzu Afcon 2025 ikiwa ni mara ya nne baada ya 1980, 2019 na 2023 ambapo nyakati zote hizo timu imeishia hatua ya makundi.

Related Posts