Dar es Salaam. Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imeweka mkazo kwenye teknolojia, vijana na kina mama ili kuhakikisha taasisi hiyo inakuwa shirikishi na kuimarisha ustawi wa wanachama wake, wengi wao wakiwa ni wafanyabiashara.
Hatua hii inalenga kutatua changamoto zinazowakabili wanachama na kuongeza ushirikishwaji wa makundi hayo muhimu.
Hayo yamebainishwa katika mkutano wa mapendekezo ya maboresho ya katiba ya TPSF uliofanyika jijini Dar es Salaam leo, Novemba 20, 2024.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Raphael Maganga amesema wanahakikisha wafanyabiashara wote wa Tanzania wanapata uwakilishi wa haki ndani ya taasisi hiyo ili changamoto zao zitatuliwe kwa ufanisi.
“Leo tumekuwa na mageuzi ya kuifanya TPSF kuwa taasisi shirikishi kwa vijana, kina mama na teknolojia. Tumepanua pia idadi ya kongani kutoka 14 hadi 25 ili kuhakikisha sekta za kiuchumi za nchi zinapata nafasi kubwa zaidi katika maamuzi ya kitaifa,” amesema Maganga.
Ameongeza kuwa, kongani zilizokuwepo awali zilikuwa chache na hazikutoa nafasi kwa wanachama wengi kuwa na wasemaji wa masilahi yao.
Kupitia ongezeko hili, wanachama sasa watapata uwakilishi bora zaidi wa kuwasilisha changamoto zao kwa Serikali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vikundi Wenye Viwanda na Biashara Ndogo Ndogo Tanzania (Vibindo), Gaston Kikuwi alieleza kuwa mageuzi hayo ni hatua muhimu kwa maendeleo ya wafanyabiashara na taifa kwa ujumla.
“Wengi wamekuwa wakiiangalia TPSF kama taasisi ya wafanyabiashara wakubwa pekee. Tunataka uwakilishi wa kila kundi—wafanyabiashara wadogo, wa kati, na wakubwa—uwepo ndani ya taasisi hii,” amesema Kikuwi.
Amebainisha kuwa wafanyabiashara wadogo wanachukua asilimia 96 ya viwanda nchini na kuchangia asilimia 66 ya ajira.
Kwa hivyo, ushiriki wao ndani ya TPSF utaongeza mchango wa mawazo na kusaidia kutatua changamoto kama vile sera, maeneo ya kufanyia biashara na huduma za kijamii.
Kikuwi pia amefichua kuwa jina la TPSF litabadilishwa kutoka taasisi kwenda kuwa shirikisho, hatua inayolenga kuondoa dhana kwamba TPSF ni taasisi ya kutoa misaada pekee.
Mwenyekiti wa Chama cha Wabunifu Tanzania, Mustafa Hassanali amesema mojawapo ya mapendekezo muhimu ni kutengeneza jukwaa maalumu kwa wabunifu.
Amesema hatua hii itasaidia kurahisisha mawasiliano ya changamoto, mapendekezo, na masuala ya kikodi kwa Serikali, pamoja na kuwaweka wabunifu kwenye dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Mwajuma Hamza amesema ongezeko la uwakilishi, ikiwemo kwa wanawake, litaimarisha uhusiano wa wafanyabiashara hao na Serikali, huku likitoa nafasi ya kushirikisha mawazo yao.
Mjumbe wa TPSF, Otieno Igogo amesema mageuzi hayo yatawasaidia wanachama wa sekta binafsi kupiga hatua kiuchumi kwa kujumuishwa na kuunganishwa zaidi na Serikali.
Mageuzi haya ya TPSF yanaonekana kuwa hatua muhimu kuelekea kuimarisha sekta binafsi nchini Tanzania, huku yakitoa fursa kwa makundi yote kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo ya kiuchumi.