MWENYEKITI wa Coastal Union anayemaliza muda wake, Steven Mguto amejiweka pembeni kwenye kinyang’anyiro cha kuwania uongozi ndani ya klabu hiyo kuelekea uchaguzi unaofanyika Desema 23 mwaka huu.
Desemba 23 mwaka huu, Coastal Union inatarajia kufanya uchaguzi mkuu wa nafasi mbalimbali ikiwemo moja ya Mwenyekiti, makamu Mwenyekiti na wajumbe saba wa kamati ya utendaji.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mguto ambaye alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo mwaka 2020, amekiri kutowania uongozi ndani ya Coastal Union huku akiweka wazi kuwa alichokifanya kimetosha sasa anawapisha wengine.
“Hadi hapo nilipofanya nashukuru, kuiongoza Coastal Union sio kitu kidogo, nimeamua kupumzika, sitakuwa sehemu ya wagombea waliopo sasa,” alisema.
Wakati Mguto akifunguka hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Coastal Union, Wakili Emmanuel Kiariro amewataja wagombea wa nafasi hiyo ya mwenyekiti kuwa ni Hassan Ramadhan Muhsin na Abdulrahman Fumbwe.
Alisema nafasi ya Makamu Mwenyekiti inagombewa na Dr. Fungo Ali Fungo na Mohammed Kiruasha Mohammed, huku nafasi ya wajumbe ikiwaniwa na watu 21 ambao ni Hussein Abdallah Moor, Khamis Seleh Khamis, Emmanuel Abdallah Mchechu, Khamis Karim Khamis, Saida Said Bawazir na Nassor Mohammed Nassor.
Wengine ni Ally Hussein Kingazi, Hafidh Nassor Suleiman, Abdullah Mbaruk Abdullah, Abdallah Zubeir Unenge, Mohammed Maulid Rajab, Baraka Mohammed Baraka, Injinia Baraka Fumbwe, Ahmed Awadh Ahmed, Salum Juma Mwawado.
Pia wapo Ally Saleh Sechonge, Omar Mtunguja Kombo, Thabit Mwinyi Abuu, Hussein Ally Mwinyihamis, Sudi Said Hilal na Wazir Mohammed Wazir. Coastal Union imekuwa na matokeo mchanganyiko katika Ligi Kuu ya Tanzania katika miaka mitano iliyopita, ikimaliza mara nyingi nafasi za kati au chini ya jedwali. Changamoto za kifedha zimepelekea katika misimu ya hivikaribuni kupoteza wachezaji wao muhimu.