Minziro akomalia nidhamu Pamba Jiji

WAKATI kikosi cha Pamba Jiji kikishuka dimbani kesho Ijumaa katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba kwenye Uwanja CCM Kirumba jijini Mwanza, kocha mkuu wa timu hiyo, Fredy Felix ‘Minziro’, amesema jambo litakalowapa ushindi ni nidhamu tu ya wachezaji.

Akizungumza na Mwanaspoti, Minziro alisema wiki mbili zimetosha kutoa nafasi kwa kila mchezaji huku jukumu kubwa ambalo amekuwa akilifanyia kazi ni kuhakikisha anatengeneza balansi nzuri kuanzia eneo lote la ulinzi na kwenye ushambuliaji.

“Kipindi hiki kimetoa nafasi kwetu kama benchi la ufundi kuangalia maeneo muhimu ya kuboresha kabla hatujarejea tena katika michezo ya ushindani, uwiano wa kufunga na kuruhusu mabao ulikuwa sio mzuri ingawa nafurahia kuna mabadiliko,” alisema Minziro.

Kocha huyo aliyewahi kuzifundisha timu mbalimbali zikiwemo Geita Gold na Tanzania Prisons, aliongeza, baada ya mchezo wa mwisho wa Novemba 5 dhidi ya Fountain Gate walioshinda mabao 3-1, uliamsha morali ya timu kiujumla.

“Bado hatupo sehemu salama kwa sababu kama unavyoona pia ushindani ni mkubwa na kila timu imejipanga vizuri, tutapambana zaidi ili kutoka chini tulipo, kufanikisha hilo ni lazima pia tujue namna nzuri ya kutatua mapungufu tuliyokuwa nayo.”

Tangu Minziro ajiunge na kikosi hicho Oktoba 17, mwaka huu akichukua nafasi ya Goran Kopunovic, ushindi na Fountain ndio wa kwanza kwake baada ya kuanza kwa sare ya 1-1 dhidi ya Kagera Sugar, kabla ya kufungwa mechi mbili mfululizo kwa bao 1-0 dhidi ya Tabora United kisha Namungo.

Pamba Jiji iliyorejea Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kupita miaka 23 tangu iliposhuka daraja mwaka 2001, inashika nafasi ya 15 kati ya 16 zinazoshiriki ligi hiyo kutokana na kushinda mchezo mmoja tu kati ya 11 iliyocheza, ikitoka sare mitano na kupoteza mitano, ikifunga mabao sita na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 13.

Related Posts