Mtikisiko unakuja Simba | Mwanaspoti

MTIKISIKO unakuja Simba ambayo ipo katika hesabu kali kuelekea dirisha dogo la usajili linalotarajiwa kufunguliwa Desemba 15, 2024.

Mabosi wa klabu hiyo wameanza mapema mikakati ya kuboresha kikosi chao kwa kufuata mapendekezo ya Kocha mkuu, Fadlu Davids, ambaye amesisitiza umuhimu wa kuziba mapengo katika maeneo kadhaa ikiwemo safu ya kiungo na ushambuliaji.

Kwa mujibu wa chanzo, inaelezwa kuwa yapo majina ya wachezaji wanne hadi sita ambayo tayari yamewekwa katika listi ya wanaoondoka baada ya tathimini ya muda mrefu iliyofanywa na kocha huyo kijana raia wa Afrika Kusini.

“Mchezaji wa kwanza kuondoka atakuwa Ngoma (Fabrice) na uzuri ni kwamba mchezaji aliomba kuondoka muda mrefu hivyo sidhani kama itakuwa ngumu kumalizana naye, wachezaji wa ndani wengi watatolewa kwa mkopo kwa sababu bado wana umri wa kukua na wanahitaji muda zaidi ya kucheza mechi za ushindani,” kilisema chanzo hicho.

Kipa Hussein Abel, ambaye Agosti mwaka huu alitimiza mwaka mmoja tangu ajiunge na Simba akitokea KMC kwa mkataba wa miaka miwili, naye ametajwa kwenye, listi hiyo.

Abel mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huku changamoto ya ushindani wa namba kikosini imekuwa ikimpunguzia nafasi ya kucheza. 

Kwa sasa Simba ina makipa sita ambao ni Moussa Camara, ambaye ni chaguo la kwanza, Ayoub Lakred aliyepona majeraha, Aishi Manula, Ally Salim, Ahmed Feruz na Hussein Abel.

Hali hiyo imeongeza presha kwa Abel, huku ikionekana kuwa nafasi yake kikosini ipo shakani. 

Mbali na Abel, mipango iliyopo ni kumuachia Manula aondoke kipindi cha dirisha dogo huku KMC ikitajwa ndiyo timu anayokwenda kuitumikia.

Uamuzi wa Aishi kuondolewa dirisha dogo unaelezwa ni shinikizo la kupata muda zaidi wa kucheza ikiwa ni sehemu ya kumuandaa kwa ajili ya kucheza michuano ya Chan itakayofanyika Februari mwakani na Tanzania itakuwa mwenyeji sambamba na Kenya na Uganda.

Kiungo Fabrice Ngoma yupo katika orodha ya wachezaji wanaoweza kuachwa. Ngoma, ambaye mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu, ameonekana kushindwa kujihakikishia nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha Fadlu.

Hata vile ambapo amekuwa akipata nafasi hivi karibuni, ilikuwa ni kutokana na majeraha ya Mzamiru Yassin na Yusuph Kagoma.

Katika nafasi anayocheza Ngoma, yupo Debora Fernandes ambaye kocha Fadlu amekuwa akimpa kipaumbele pia Augustine Okejepha, naye bado anajitafuta kikosini licha ya kwamba amecheza zaidi kuliko Ngoma.

Aidha, suala la umri wa Ngoma, ambaye sasa ana miaka 30, linaonekana pia kuwa sababu kubwa ya viongozi wa klabu hiyo kubariki kuondoka kwake hiyo inatokana na kuwa na mikakati ya muda mrefu ndiyo maana asilimia kubwa ya wachezaji waliosajiliwa kipindi cha dirisha kubwa msimu huu ni chini ya miaka 30. 

Katika safu ya ulinzi, Hussein Kazi naye anakabiliwa na wakati mgumu mbele ya mabeki wengine kama Che Malone Fondoh, Abdulrazack Hamza na Chamou Karaboue.

Wachezaji hao wamekuwa wakipata nafasi mara kwa mara, huku Kazi akikosa muda wa kutosha uwanjani. Kabla ya msimu kuanza, Kazi alikuwa akihusishwa na mpango wa kutolewa kwa mkopo, lakini nafasi hiyo haikufanikiwa. 

David Kameta pia ameorodheshwa kuwa hatarini kuachwa kutokana na kushindwa kutoa ushindani kwa Shomary Kapombe katika nafasi ya beki wa kulia.

Hali ni tofauti kwa Kelvin Kijili, ambaye ameonyesha kiwango kizuri na changamoto katika nafasi hiyo. 

Omary Omary, kiungo wa kati, naye anaweza kujikuta akitolewa kwa mkopo ili kupisha nafasi ya wachezaji wapya. Hali yake ya kutopata muda wa kutosha wa kucheza akitumika katika mechi moja pekee ya ligi tena kwa dakika 23, inamfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaoweza kuondolewa kwa mpango wa muda au wa kudumu. 

Kocha Fadlu anadaiwa kueleza kuwa mabadiliko hayo kwa mujibu wa chanzo hayalengi tu kupunguza wingi wa wachezaji bali pia kuongeza ubora wa kikosi.

Kwa sasa, Simba inataka wachezaji watakaolingana na mahitaji ya mfumo na falsafa ya uchezaji ya kocha huyo. 

Lengo kuu la Simba katika dirisha dogo ni kuimarisha safu ya kiungo na ushambuliaji, hasa baada ya changamoto za muda mrefu zinazokikabili kikosi hicho katika maeneo hayo. Kwa mujibu wa taarifa, tayari majina kadhaa ya nyota wapya yamependekezwa kwa mabosi wa klabu hiyo.

Mbali na kusajili wachezaji wapya, klabu pia inatazamia kuwaweka baadhi ya wachezaji wake wa sasa kwa mpango wa mikopo ili kuwapa nafasi ya kucheza mara kwa mara katika timu nyingine. 

Dirisha dogo linatarajiwa kuwa muda wa mabadiliko madogomadogo ndani ya kikosi cha Simba, huku mashabiki wakiwa na matumaini ya kuona timu yao ikipata nguvu mpya itakayowasaidia kufanikisha malengo ya msimu huu. 

Kwa upande mwingine, wachezaji waliopo kwenye hatari ya kuondolewa wana kazi ya kuonyesha kiwango bora zaidi kabla ya dirisha dogo kufunguliwa ili kujaribu kujihakikishia nafasi zao kikosini. 

Katika kipindi hiki, Simba inalenga kuhakikisha kuwa kikosi kinakuwa na wachezaji walio bora, wenye uwezo wa kushindana katika ngazi za juu na kufanikisha ndoto za klabu hiyo. 

Ikiwa na shauku ya kurejesha heshima yao katika ligi mbele ya mtani wao Yanga lakini pia na kufanya vizuri katika Kombe la Shirikisho Afrika. Kwa sasa Simba inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 25, wapo juu kwa tofauti ya pointi moja na Yanga ambao wapo nafasi ya pili baada ya timu hizo kucheza mechi 10 kila moja.

Related Posts