Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali haitasita kubomoa majengo yote ya Kariakoo iwapo tume iliyoundwa kuchunguza usalama wake, itashauri ifanyike hivyo.
Sambamba na hilo, mkuu huyo wa nchi amewasihi watendaji wa Serikali kuwajibika kwa nafasi zao, hasa katika mchakato wa utoaji vibali vya ujenzi akitaka visimamiwe.
Rais Samia ameyasema hayo siku nne tangu lilipotokea tukio la kuporomoka kwa jengo la ghorofa nne Kariakoo jijini Dar es Salaam na kusababisha vifo 20 hadi leo saa 3 asubuhi.
Tukio hilo, lililotokea wakati mkuu huyo wa nchi akiwa njiani kwenda Rio De Janeiro nchini Brazil alikoalikwa kuhudhuria mkutano wa G20, uliofanyika kati ya Novemba 18 na 19, 2024 limesababisha majeruhi zaidi ya 80.
Hata hivyo, tayari Rais Samia alishamtaka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuongoza uchunguzi wa majengo yote ya Kariakoo na mengine yote kujua usalama wake sokoni hapo.
Mbali na tume, pia aliagiza mmiliki wa jengo lililoporomoka ahojiwe na kuongeza siku za uokozi kutoka saa 72 hadi 96.
Rais Samia ameyasema hayo Kariakoo jijini Dar es Salaam leo Jumatano, Novemba 20, 2024 alipotembelea eneo la tukio, saa chache baada ya kuwasili nchini akitokea Brazil. Baada ya kutoka Kariakoo alikwenda Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kuwajulia hali na kuwapa pole majeruhi.
Rais aliagiza iundwe tume kuchunguza majengo yote ambapo tayari Majaliwa ameunda ikiwa na wajumbe 19, akibainisha kuwa matokeo yatakayopatikana yatawekwa wazi kwa wananchi.
Pamoja na kuwekwa wazi, ameeleza iwapo tume hiyo itashauri majengo yote sokoni hapo yavunjwe, hatasita kufanya hivyo.
“Sasa tume imeona nini, imesema nini, imetushauri nini, kama tume itatushauri tuendelee kubomoa majengo yasiyokuwa na sifa hatutasika kufanya hivyo. Kwa hiyo hatua zote ambazo tume itatushauri hatutasika kufanya hivyo,” amesema.
Rais Samia amesema anatambua uwepo wa ripoti za tume mbalimbali ikiwemo ya mwaka 2013, akisema uchunguzi unaofanywa utazingatia pia mapendekezo ya tume hiyo.
Tume ya mwaka 2013, iliundwa Machi 29, mwaka huo baada ya jengo la ghorofa 16 katika makutano ya barabara za Zanaki na Indira Ghandi kuanguka na kupoteza uhai wa watu 36.
Hatua hiyo ilisababisha kampuni ya Design Plus Architects (DPA) kupewa zabuni ya kukagua majengo Manispaa ya Ilala kujua usalama wake na Novemba 5, 2013, ilitoa ripoti yake.
Katika ripoti hiyo, DPA iliweka wazi kuwa, kati ya maghorofa 90 yaliyokaguliwa, 67 yalijengwa kinyume cha sheria.
Kampuni hiyo ilisema baadhi ya majengo hayo yanaweza kuporomoka kutokana na ujenzi wake kuwa chini ya kiwango.
Aidha, kufuatia jengo hilo kuporomoka, aliyewahi kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na mkurugenzi wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-Habitat), Profesa Anna Tibaijuka, kupitia mtandao wa kijamii wa X alindika:
Kwa sheria za mipango miji ilitakiwa viwanja vinne vya ‘high density’ viunganishwe mbele na nyuma kipatikane kiwanja kimoja kikubwa cha kujenga ghorofa imara yenye ‘basement’ kubwa kupaki magari.
Ghorofa inayofunguka kwenye mtaa wa mbele na nyuma awali katika awamu ya tatu ushauri huo wa wataalamu wa mipango miji ulishapuuzwa na viongozi kwa presha ya wawekezaji, kwa hiyo maghorofa Kariakoo na kwingineko yanajengwa kiholela kwenye viwanja visivyokidhi vigezo.
Pamoja na madhaifu ya usimamizi wa ujenzi kiuhandisi ni vigumu majengo kuwa imara bila kuwa na eneo la kutosha kujenga kitako yaani ‘base foundation’ stahiki. Naendelea kuhimiza kurekebisha kosa hilo.
Sasa tunavuna hasara kubwa ya upotevu wa mali, maisha na fursa za ajira na aibu ya kushindwa kusimamia viwango vya ujenzi miaka 63 baada ya uhuru. Naendelea kushauri viwango vya ‘vertical development’ vizingatiwe kuanzia sasa. Tujisahihishe.
Kwa mtazamo mwingine wa kitaalamu, msingi wa ghorofa unapaswa kujengwa kuhimili uzito wa jengo na vitakavyofanyika ndani yake, ikifanyika kinyume chake lazima litaanguka.
Inaelezwa baadhi ya maghorofa yamejengwa kwa matumizi ya hoteli na makazi, lakini yamebadilishwa matumizi na kuhifadhi mizigo, jambo linaloweza kusababisha kuporomoka.
Mhandisi wa Ujenzi, Joseph Rwihura akizungumza na Mwananchi hivi karibuni baada ya jengo hilo kuporomoka amesema ukiukwaji wa viwango vya msingi wa ghorofa inaweza kuwa sababu ya kuporomoka.
Amesema ujenzi wa ghorofa huanza na msingi unaojengwa kwa uimara kwa kuzingatia idadi ya ghorofa zitakazobebwa na jengo husika.
“Kama jengo litakuwa na ghorofa mbili, basi msingi utajengwa kwa uimara utakaomudu kubeba ghorofa mbili. Kwa bahati mbaya majengo mengi Kariakoo, misingi yake imejengwa kubeba kiwango fulani cha ghorofa, lakini mahitaji yanasababisha watu wanaongeza ghorofa juu ya jengo,” amesema.
Kubadilishwa matumizi ya jengo ni sababu nyingine akieleza kwa uhalisia wa Kariakoo, majengo mengi yalijengwa kuwa makazi ya watu na hoteli, lakini yanatumika kuhifadhi mizigo zikiwemo mashine na mitambo.
“Jengo lililojengwa kwa matumizi ya makazi, halipaswi kutumiwa kuhifadhi mtambo au mizigo. Ukifanya hivyo linazidiwa uwezo na utafika wakati litaanguka,” amesema.
Katika hotuba yake hiyo kwa wafanyabiashara wa Kariakoo, Rais Samia amewataka watendaji wa Serikali kuhakikisha wanatimiza wajibu wao hasa wale wanaohusika na utoaji wa vibali vya ujenzi.
Amesema ukiangalia kwa macho, tukio hilo linaashiria kuwepo kwa upungufu wa utendaji na uwajibikaji kwa baadhi ya watendaji.
“Bila shaka jengo hilo lilipata vibali kutoka halmashauri na serikalini kwa ujumla, lakini vibali ni jambo moja, usimamizi ni jambo jingine. Jengo lile halikutizamwa ubora wake wakati wa ujenzi. Niwaombe watu wote tunaohusika tuseme kwa pamoja matukio ya aina hii yasijirudie,” amesema.
Hata hivyo, ameeleza kwa kuangalia inaonekana jengo halikuwa limesimamiwa vema na kwamba hilo limewapa funzo la kuangalia majengo yote ya Kariakoo,” kwamba Serikali sasa tuingie Kariakoo na kuangalia majengo.”
Ameeleza kufurahishwa na hatua ya kutekelezwa kwa maelekezo yake ya kuundwa kwa tume ya watu 20, aliosema wanasubiri maelekezo waanze kazi.
Baada ya hatua za uokoaji kukamilika, Rais Samia amesema eneo hilo litafungwa kuiruhusu usafi ufanywe na miili itakayopatikana istiriwe.
Kwa sababu hiyo, amesema wafanyabiashara wa maeneo ya jirani watalazimika kufunga biashara zao, huku waliopo mbali na hatari hiyo akitaka waendelee na shughuli zao.
Wakati wa usafi katika jengo hilo, amesema bidhaa na mali zote zilizopo ndani zitapelekwa ghalani kuhifadhiwa na baadaye wamiliki wataitwa kuzitambua na kukabidhiwa.
Ameeleza kufurahishwa na hatua ya vikosi vya ulinzi na usalama na wananchi walivyoshirikiana kuokoa waathirika.
“Kazi tuliyoifanya kama Watanzania ni kubwa iliyofanywa kwa ushirikiano ili kuwanusuru wenzetu,” amesema.